Michezo

Warsha kuandaliwa kuelimisha timu za KPL msimu mpya ukinukia

October 23rd, 2018 1 min read

Na CECIL ODONGO

KAMPUNI inayoendesha ligi kuu nchini KPL inapanga kuandaa warsha ya siku moja kwa klabu zote 18 zitakazoshiriki KPL msimu wa 2018/19 Ijumaa Novemba 2.

Kamati ya KPL inayosimamia maswala ya matibabu na hali ya afya ya wanaasoka wanaowajibikia ligi hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wake Dkt Andrew Suleh amesema kwamba warsha hiyo itaandaliwa kwenye makao makuu ya KPL mtaani Westlands viungani mwa mji wa Nairobi.

Msimu wa 2018/19 unatarajiwa kuanza Jumamosi Disemba 8 kinyume na miaka ya nyuma ambapo msimu huo ulianza mwezi Februari. Hii itahakikisha KPL inaendelea sambamba na ligi nyingine mashuhuri duniani.

Miongoni mwa klabu zinazotarajiwa kushiriki warsha hiyo ni Kcb na Western Stima ambao walifuzu kushiriki KPL kutoka ligi ya Kitaifa ya Supa(NSL) baada ya kumaliza katika nafasi za kwanza na pili mtawalia.

Ushuru FC na Nakumatt FC vile vile wanatarajiwa kushiriki mkondo wa pili wa mechi ya kuamua mshiriki wa tatu wa KPL kati ya timu iliyoepuka shoka la kutimuliwa na ile iliyomaliza katika nafasi ya tatu  NSL Jumapili Oktoba 28. Nakumatt wapo guu moja ndani kutwaa nafasi hiyo baada ya kushinda mkondo wa kwanza 1-0.