Dondoo

Warudi na mahari kwa kukosa ugali

December 5th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

KOYONZO, VIHIGA

KIOJA kilizuka kijijini hapa baada ya wazee kuamua kurudi nyumbani na mahari waliyokuwa wameleta, wakidai hawakupokelewa vizuri na wakwe zao.

Inasemekana wazee hao hawakufurahishwa na namna familia ya msichana iliandaa hafla hiyo maalum. Kulingana nao, hawakupewa mapokezi yaliyostahili ujumbe wao.

Duru zilizotufikia zinadai kuwa, wazee wa upande wa msichana hawakuwepo kuwapokea wazee wenzao walipowasili.

Wageni hao wakaamua kusubiri wakati mwafaka kulalamika. Baada ya muda mfupi, vyakula viliandaliwa kabla ya majadiliano na hapo ndipo kitumbua kiliingia mchanga.

Wazee walianza kunong’onezana kwa sauti ya chini. Vijana walioandamana nao pia walianza kuangaliana.“Mlo ni huu pekee ama kuna mwingine!” mzee mmoja akainuka.

Wenyeji walijaribu kubembeleza wageni waanze kula, lakini hakuna aliyesongeza karibu sahani yake. “Hawa vijana wametembea mwendo mrefu sana.

Wanataka kujua iwapo kuna ugali mwingine ama ni huu peke yake,” mzee huyo akasisitiza. Wenyeji walibaki vinywa wazi.

“Kidesturi, sisi hula ugali sampuli tatu katika hafla za kitamaduni kama hizi. Ugali wa mahindi, wa mhogo na wa wimbi. Nyama nayo lazima iwe kwa wingi,” mkongwe huyo aliendelea kunena huku vijana wakimpongeza.

Wenyeji walijitetea kuwa hawajui mila hiyo, na kwamba wageni wanafaa kula chochote walichoandaliwa.

“Hatuwezi kuwaletea ng’ombe na mbuzi hao wote halafu nyinyi mnatuandalia mlo ambao hatuwezi kushiba,” mzee mwingine akawafokea wakwe hao.

Wazee waliamka kwa pamoja na kuelekea walikokuwa mifugo wao. “Hii bado ni mali yetu na tunarudi nayo nyumbani. Tutakula huko!” wazee waliapa.

Walianza safari kurudi nyumbani. Familia ya msichana ilijaribu kuwashawishi waketi chini lakini wapi.

“Kuleni mlo wenu. Sisi si watoto wa kuletewa wali kwa supu. Mkiwa tayari kutupokea mtuarifu,” wazee walifoka huku wakienda zao.