WARUI: Serikali iharakishe maandalizi ya sekondari kwa CBC

Na WANTO WARUI

HUKU ukibakia mwaka mmoja na miezi michache tu ili wanafunzi wa Gredi ya 5 watamatishe elimu yao ya shule ya msingi na kujiunga na sekondari, dalili za ni wapi wanafunzi hao watakakosomea masomo yao ya sekondari bado hazijaonekana.

Ijapokuwa kuna tetesi kwamba shule za sekondari katika Gredi ya 7 hadi 9 zitashirikishwa pamoja na zile za msingi, jambo hili lingali usiku wa giza kwa watu wengi.

Mpango wa ni wapi shule hizo zitakapokuwa na majengo ya madarasa yao pamoja na maabara za kufanyia tafiti mbalimbali unastahili kuwa umeshika kasi kufikia sasa.

Matayarisho kabambe yanahitajika ili kuwezesha mfumo huu kufaulu. Kwa mfano, mbali na madarasa ya kusomea na maabara ya shule za sekondari za hapo awali, mfumo huu unahitaji maabara mengine pamoja na stoo kadhaa.

Kuna Somo la Sayansikimu ambalo masomo yake ni ya utendaji zaidi kuliko nadharia; upishi, vyombo vya mapishi na viungo vyake, mashine za kushonea na za kufumia sweta ni baadhi tu ya vitu vinavyohitaji kutengewa nafasi.

Somo la sanaa nalo linashughulikia masuala ya uchongaji, uchoraji na ufinyanzi miongoni mwa mambo mengine. Kuna Somo la Muziki ambalo litahitaji kuwa na ukumbi wake wa kuhifadhia ala za muziki. Somo la Kilimo lina sehemu kubwa sana ya kushughuliwa ikiwemo vipande vya shamba, ufagaji wa wanyama kama vile sungura na kuku miongoni mwa mambo mengine.

Kutokana na shughuli nyingi ambazo zinatarajiwa kuwa katika shule za sekondari, mipango madhubuti haina budi kuwekwa mapema. Vifaa vya kutosha vya kukuzia talanta vinafaa kuwepo shuleni, walimu wenye ujuzi wa kutosha katika nyanja mbalimbali za masomo, madarasa na maabara ya kusomea. Kuwaweka walimu, wazazi na washikadau wengine gizani mpaka dakika za mwisho kutaharibu mambo na kuzua mshikemshike siku za mwisho.

Taharuki

Maelfu ya walimu, wazazi na wanafunzi walio katika Gredi ya 5 sasa wana wasiwasi kwani hawajui wanakoelekea. Wanasubiri tu maagizo ya Wizara ya Elimu ambayo hayaonekani kama yatatolewa hivi karibuni.

Kufikia sasa ambapo asilimia sabini ya masomo katika shule za msingi ni CBC, kuna baadhi ya shule ambazo hazijapambanukiwa na mtaala huu na zingali zinaendeleza masomo zikitumia mfumo wa 8-4-4. Wanafunzi ambao wanajipata katika shule kama hizi watakuwa na kibarua kigumu kujiandaa kuingia shule za sekondari.

Kuna haja kubwa sana kwa serikali kuweka mipango madhubuti mapema na kuwajuza washikadau wote mapema ili kuweza kujitayarisha. Kusubiri mpaka mwaka wa kujiunga na sekondari ufike hakutasaidia ila kutasababisha wasiwasi shuleni, kwa wazazi na washikadau wengine.

Habari zinazohusiana na hii