Wasafiri wataka ujenzi wa Uwanja wa Ndege Manda ukamilishwe

Wasafiri wataka ujenzi wa Uwanja wa Ndege Manda ukamilishwe

NA KALUME KAZUNGU

WASAFIRI wanaotumia uwanja mdogo wa ndege wa Manda, Kaunti ya Lamu wameitaka serikali iharakishe ujenzi wa kuupanua.

Wasafiri hao wamelalamika kuwa wao huchafuka kwa tope wanaposhuka kutoka kwa ndege wakati inaponyesha.Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA), ililazimika kutenga sehemu mbadala na ya muda ya ndege kutua na kupaa katika uwanja huo ili kutoa nafasi ya ujenzi kuendelezwa.

“Unatoka kwako ukiwa msafi. Punde unaposhuka uwanja wa Ndege wa Manda unapata vidimbwi vya maji na tope kila mahali,” akasema Bi Faith Akinyi, msafiri.

Wakati wa ziara yake Lamu mnamo Septemba 2021, Katibu wa Wizara ya Uchukuzi na Miundomsingi, Bw Solomon Kitungu, aliahidi kwamba, ujenzi wa uwanja huo ungekamilika kufikia Novemba 2021.

Afisa katika uwanja huo aliyeomba asitajwe jina, kwa vile hana mamlaka kuzungumzia masuala ya ujenzi wake, alisema ujenzi umekamilika kwa asilimia 75.

“Huu ni msimu wa mvua na ni vigumu kwa mwanakandarasi kuendeleza ujenzi. Mradi uko asilimia 75 hivi. Pia tumekuwa tukikumbwa na uhaba wa maji uliochangia kucheleweshwa kwa mradi,” akasema afisa huyo.

Meneja wa KAA anayesimamia Pwani, Bw Peter Wafula, hakuweza kutoa kauli yake mara moja, akisema kuwa yuko mkutanoni na atazungumzia suala hilo baadaye.

  • Tags

You can share this post!

PAA yajipata pabaya Jumwa akikaa ngumu

Ruto aahidi atakubali matokeo akishindwa

T L