Habari Mseto

Wasafiri waumia mabasi ya Modern Coast yakizimwa

December 12th, 2019 2 min read

MISHI GONGO na PIUS MAUNDU

MAMLAKA ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA), Alhamisi ilikiri kupokea malalamishi kuhusu mabasi ya kampuni ya Modern Coast kabla ajali kufanyika na kusababisha vifo vya watu watano.

Kwenye taarifa, Mkurugenzi Mkuu wa NTSA Bw George Njao alisema shirika hilo limekuwa likifuatilia mabasi hayo kwa karibu, kufuatia ripoti za wananchi kuhusu matukio kadhaa ya kunusurika kogangana na mabasi mengine awali.

Haijajulikana wazi kwa nini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi ajali ikatokea jana alfajiri ikihusu mabasi mawili ya kampuni hiyo yaliyogongana na kusababisha vifo vya watu watano huku wengine 62 wakijeruhiwa.

“Kwa siku kadhaa sasa, shirika hili limekuwa likifuatilia kwa makini huduma za kampuni ya Modern Coast Limited baada ya ripoti kuhusu ajali kadhaa ambazo watu walinusurika kifo,” akasema, akitangaza kwamba mabasi hayo yamepigwa marufuku kwa muda.

Wasimamizi wa Modern Coast walisema watakutana na NTSA leo kutafuta mwafaka kuhusu marufuku hiyo ambayo imewaacha wasafiri wengi bila namna huku wakiahidi kurudishia wateja wao nauli ambazo walikuwa washalipa.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kiongwani, barabara kuu ya Mombasa-Nairobi, eneo ambalo limetajwa kuwa hatari mwaka huu, baada ya ajali zaidi ya 10 kutokea ndani ya wiki tatu zilizopita.

Abiria 50 walipata majeraha madogo huku 17 wakijeruhiwa vibaya. Majeruhi walipelekwa katika hospitali za Kaunti ya Machakos na Makueni.

“Basi moja lilikuwa linaelekea Malaba jingine likielekea Nairobi. Basi lililokuwa likitoka Mombasa lilitoka katika barabara yake na kugongana na lile lililokuwa likitoka Malaba,” alieleza kamanda wa polisi kaunti ya Makueni Ole Napeiyan.

Waliofariki walijumuisha dereva wa mabasi hayo na mtoto wa miaka miwili. Miili ya wendazao ilipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali kuu ya Machakos.

Mamia ya abiria walitatizika katika vituo vya mabasi vya kampuni hiyo vilivyo miji tofauti ya nchi.

Mjini Mombasa, abiria ambao walifaa kusafiri jana asubuhi walibaki wameduwaa wasijue la kufanya, wakisubiri maelekezo kutoka kwa usimamizi wa shirika hilo.

Kituo hicho kililindwa na maafisa wanne wa polisi kuhakikisha kuwa hakuna basi linalosafiri kama walivyoelekezwa na NTSA.

Abiria mmoja, Bi Miriam Maingi ambaye alipaswa kusafiri na gari la saa mbili, alieleza hali ya kukerwa kufuatia usimamizi wa Modern Coast kutowapa taarifa kuhusiana na tatizo hilo.

“Nimefika hapa saa moja, niko na watoto, kila tunapowauliza kuhusu usafiri wetu hawatujibu wanatuambia tusubiri. Sasa hivi ni saa nne na hatujaambiwa kitu,” akasema.

Mwengine ambaye alidai alikuwa anasafiri kwenda kwa matibabu katika hospitali kuu ya Kenyatta.

“Sina uwezo wa ndege, treni zimejaa, nisiposafiri leo nitapoteza nafasi yangu ya kupokea matibabu,” akasema.

Gorge Otieno, alisema kusimamishwa kwa huduma za shirika hilo,kumewaathiri pakubwa hasa wafanyi biashara ambao wanatumia mabasi hayo kusafirisha mizigo.

“Niko na bidhaa ambazo zinafaa kufika Nairobi leo jioni,nishalipa ada husika lakini hadi sasa sijapatiwa usafiri,” akaeleza.

Anwar Juma alisema wanatarajia shirika hilo litatatua tatizo hilo kwa haraka na wataangalia maslahi ya abiria wao.

“Wakishindwa kutatua, watutafutie njia mbadala ya usafiri,” akasema.