Habari Mseto

Wasahihishaji wa KCSE waikejeli KNEC kutowalipa hela za 2017

March 12th, 2018 1 min read

Na ELIZABETH OJINA

WALIMU kutoka kaunti ya Kisumu wametishia kugomea usimamizi na usahihishaji wa mitihani mwaka huu, iwapo hawatalipwa pesa za mwaka 2017 ambazo wanadai.

Kupitia chama cha walimu wa taasisi za masomo ya juu (KUPPET), wamelishutumu baraza la mitihani nchini (KNEC) kwa kukosa kuwalipa pesa zao jumla ya Sh1.5 bilioni zinazopaswa kuwa ujira kutokana na kusahihisha mitihani ya mwaka jana.

Katibu Mkuu wa KUPPET tawi la Kisumu, Bw Zablon Awange alikiri kuwa walimu hao walisema kwamba malipo hayo yalijumuishwa kwenye bajeti ya KNEC na kupangwa kuwa ya kulipwa wasahihishaji hata kabla ya mtihani wa 2017 kuanza.

“Sisi viongozi wa chama tunasikitishwa na tabia ya KNEC kukataa kuwalipa walimu ambao walisahihisha KCSE, miezi minne baada ya matokeo ya mtihani huo kutolewa.

Kama KNEC haiwezi kuwalipa walimu, basi yafaa iajiri wasahihishaji wake, ambao watakuwa wakitekeleza majukumu bila kutarajia kulipwa,” akasema.

Lakini Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa KNEC, Bi Mercy Karogo alisema jumla ya watahini 9,000 wameshalipwa Sh581milion na kwamba wale ambao hawajalipwa ni 230 pekee.