Washukiwa 16 wakamatwa kwa kuitisha wakazi Mukuru pesa

Washukiwa 16 wakamatwa kwa kuitisha wakazi Mukuru pesa

Na SAMMY KIMATU

NAIROBI

WATU 16 walikamatwa kwa kushukiwa kuwatoza raia pesa kwa lazima katika mitaa ya mabanda katika kaunti ya Nairobi mwishoni mwa wiki.

Mkuu wa polisi eneo la Makadara, Bw Timon Odingo alisema washukiwa, wote wanaume walilazimisha wakazi katika mitaa ya mabanda ya Lunga Lunga na Sinai. Mitaa yote miwili imo katika wodi ya Viwandani kwenye kaunti ndogo ya Makadara.

“Washukiwa walilazimisha wakazi kuwapatia pesa baada ya kuunganishiwa stima kinyume cha sheria. Pia walilazimisha wahudumu wa matatu kulipa ‘ada’ ya kubeba wateja katika steji za matatu mkabala wa barabara ya Lunga Lunga,’’ Bw Odingo akaambia Taifa Leo.

Fauka ya hayo, ripoti za majasusi zilisema watu fulani wamejipanga kuzua rabsha kabla, wakati na baada ya uchaguzi ujao mwaka 2022. Aidha, Bw Odingo alifafanua kwamba polisi wako macho kuzima vitendo vya uhalifu katika maeneo yanayoaminika kuwa ngome ya ghasia kila wakati tunapokaribia uchaguzi mkuu.

“Nia ya msako wetu ni kuwakabidhi kisheria watu wote wanaopanga kuzua rabsha tukikaribia uchaguzi mkuu. Tuna habari kutoka mashinani ndiposa tumeanzisha misako katika kila mtaa wa mabanda Mukuru kuwakamata wanaohusika,’’ Bw Odingo akanena.

Isitoshe, ametoa wito kwa vijana kukataa kutumiwa na wanasiasa kusababisha ghasia raundi hii na badala yake kutoa ripoti kwa vitengo vya usalama ili wahusika wakabiliwe kwa mujibu wa sheria. Bw Odingo aliongeza kwamba washukiwa hao wamejipanga kwa makundi huku wakitembea nyumba hadi nyumba wakiitisha pesa kama ilivyokuwa kwa kundi haramu la mungiki hapo awali.

“Makundi hayo ni sawa na lililokuwa la Mungiki amabapo wanaitisha pesa za stima mitaani, ushuru kwa matatu kubeba wateja katika steji na kubeba wateja kwa bodaboda katika maeneo mbalimbali kilazima,” Bw Odingo akanena.

You can share this post!

Wawili waponea kifo kwa pikipiki Mukuru Kayaba

FAUSTINE NGILA: Afrika isipojipigia debe Wikipedia...

T L