‘Wasanii Wazoefu’ mboni ya sanaa chuoni Gretsa, Thika

‘Wasanii Wazoefu’ mboni ya sanaa chuoni Gretsa, Thika

Na CHRIS ADUNGO

KATIKA jitihada za kujiboresha na kujiimarisha kielimu pamoja na masuala yasiyo ya kiakademia, Chuo Kikuu cha Gretsa mjini Thika kinajivunia kundi maarufu la ‘Wasanii Wazoefu’.

Kundi hili liko chini ya mwavuli wa kundi la ‘Wanajopo wa Chuo Kikuu cha Gretsa’ ambalo linachapukia zaidi shughuli za makuzi ya lugha na sanaa ya maigizo.

Wanajopo wa Gretsa ni kundi lililoanzishwa mwaka wa 2015 chini ya ulezi wa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Gretsa, Profesa Kuria Thuo ambaye anaunga mkono kikamilifu mikakati na harakati zote za Jopo. Juhudi za Prof Thuo zinapigwa jeki na Bi Stella Marete ambaye ni Mudiri wa Wanafunzi chuoni.

Bw George Mulama naye yuko mstari wa mbele kuendesha kundi hili kuandaa maonyesho mbalimbali kwa usaidizi wa Bw Hezron Manyasi ambaye ni mkutubi mkuu wa chuo.

Chuo Kikuu cha Gretsa kinafundisha kozi mbalimbali katika mawanda ya lishe, sayansi na teknolojia, uanahabari, uhandisi, ualimu miongoni mwa taaluma nyinginezo.

Jopo la Gretsa linajivunia takriban wanajopo 200 na linawajumuisha baadhi ya wanafunzi wanaosomea taaluma ya ualimu, hususan somo la Kiswahili. Wanafunzi wa taaluma nyinginezo pia wana uhuru wa kujiunga na kundi hili.

Vinara wa Jopo kwa sasa ni Collins Gichuki (Mwenyekiti), Simiyu Nasimiyu (Naibu Mwenyekiti), Kerubo Mang’era (Mhazini), Wanasamba Solomon (Katibu Mratibu) na Bw Korir ambaye ni mlinda maslahi ya wanafunzi.

Wanajopo huhamasisha jamii kuhusu masuala muhimu kupitia michezo ya kuigiza katika Kiswahili na mashairi.Baadhi ya michezo yao iliyojizolea tuzo kemkem kwenye tamasha za kuigiza chini ya uelekezi wa Bw Mulama ni ‘Tandabelua Latanda’ (2016), ‘Chanjo Chungu’ (2017), ‘Barafu Moto’ (2018), ‘Nzige Bungeni’ (2019).

Vipaji vya kusakata densi, kuimba, kuigiza pamoja na kutunga, kukariri na kughani mashairi vimeimarika sana miongoni mwa wanafunzi wa Gretsa kupitia kundi la Wasanii Wazoefu.

Chuo Kikuu cha Gretsa kimeibuka cha kwanza mara si mosi katika mijadala ya Kiswahili miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu mbalimbali.

Wanajopo kwa sasa wako tayari kufyatua mchezo wa kuigiza wenye mada ‘Barakoa ya Chuma’ na mashairi yenye mada ‘Supu ya Sima’, ‘Maskini Maarufu’ na ‘Olisikia Wapi?’Baadhi ya wanajopo pia wanaendelea kuandika riwaya ‘Chozi la Samaki’ na diwani ‘Kiberiti Kimeloa’ chini ya uelekezi wa Bw Manyasi na Bw Mulama.

Kubwa zaidi katika maazimio ya kundi hili ni kuanzisha ‘Gretsa Theatre Troupe’ kwa nia ya kuigiza vitabu teule vinavyotahiniwa katika shule za sekondari nchini Kenya.

You can share this post!

Sifa zinazozolea kanga umaarufu

Mashine zapokonya wachunaji majanichai kazi