Washirika wa Ruto Mlimani wamtetea Waiguru

Washirika wa Ruto Mlimani wamtetea Waiguru

DPPS na BENSON MATHEKA

WASHIRIKA wa Naibu Rais William Ruto kutoka eneo la Mlima Kenya sasa wamemtetea Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru, na kuitaka serikali kukoma kumhangaisha kwa kujiunga na chama cha United Democratic Alliance (UDA).

EACC ilikuwa ikimchunguza Bi Waiguru hata kabla ya kuhamia UDA japo amekuwa akidai inamuandama kwa kuhama Jubilee. Wakizungumza jana katika makazi rasmi ya Dkt Ruto, wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Irungu Kang’ata ( seneta, Murang’a), Kimani Ichung’wah (Kikuyu), Alice Wahome (Kandara), Jayne Kihara (Naivasha), Rigathi Gachagua (Mathira) na Faith Gitau (Nyandarua) walilaumu EACC na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa kutumiwa kuandama wanaokataa kumuunga kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga.

“Nyinyi (EACC na DCI) mnakosa maadili haraka sana, kwa kuwa mumekubali kutumiwa kutimiza malengo ya kisiasa,” akasema Bw Nyoro. Alisema kwamba, vitisho kutoka kwa EACC na DCI havitawafanya waache mpango wao wa kuwezesha kiuchumi mamilioni ya Wakenya masikini.

Bw Kang’ata alidai EACC inalinda wanasiasa fisadi wanaomuunga Bw Odinga. Kinaya ni kwamba, viongozi hao walikuwa wakimshambulia Bi Waiguru kwa madai ya kuhusika na ufisadi kabla yake kuhamia UDA.

Hata hivyo, hawakutoa ushahidi kwamba EACC na DCI zinatumiwa kuhangaisha wanaokataa kumuunga Bw Odinga. Walimhimiza Bi Waiguru kutotishika na kumtaka akae ngumu katika UDA.Dkt Ruto aliwataka wanasiasa kuepuka siasa za kikabila na kuungana kubadilisha maisha ya Wakenya.“Uchaguzi mkuu ujao utahusisha uchumi.

Wakenya wanatutaka kuwapa ajenda na wako tayari kutusikiliza,” alisema. Aliwataka viongozi wa kisiasa kukumbatia siasa za kitaifa na sio kugawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila.

You can share this post!

Kafyu ilizamisha mabilioni ya pato la kaunti -Ripoti

Muturi atetea MCAs kuhusu digrii

T L