Siasa

Washirika wa Uhuru, Raila wataka IEBC ipewe pesa

December 13th, 2020 1 min read

Na PATRICK LANG’AT

WABUNGE wanaoegemea mrengo wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga, sasa wanaitaka Wizara ya Fedha itoe pesa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili mchakato wa kuthibitisha saini zilizowasilishwa kuunga ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) uanze mara moja.

Wanasiasa hao walisema hiyo ndiyo njia pekee ya kuhakikisha kura ya maamuzi inayotarajiwa kuandaliwa kufikia Aprili 2021 haicheleweshwi.

Baada ya kupokezwa saini hizo na sekreteriati ya BBI inayoongozwa na Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na mbunge wa zamani wa Dagorreti Kusini Dennis Waweru, IEBC ina miezi mitatu pekee kuzithibitisha kama zitafika milioni moja zinazohitajika kisheria kuunga mswada wa BBI.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alipokuwa akipokea saini hizo alisema tume haina fedha na itaanza shughuli hiyo rasmi baada ya kupokea hela kutoka Wizara ya Fedha.

Mwenyekiti wa kamati ya bajeti bungeni Kanini Kega alisema wizara ya fedha inaruhusiwa kutoa pesa za matumizi kwa masuala muhimu kitaifa kama BBI kisha kufahamisha bunge na kujumuisha matumizi hayo kwenye bajeti ya ziada itakayowasilishwa wabunge wakirejelea vikao mwakani.

Hata hivyo, mbunge huyo wa Kieni alisema IEBC haihitaji pesa nyingi kuthibitisha saini hizo jinsi inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa.

“Kile IEBC inahitaji si fedha nyingi. Tayari wana wafanyakazi na vifaa vya kufanya kazi na wanahitajika tu kuwaongeza wafanyakazi wachache. Kwa hivyo, ukosefu wa fedha haufai kuwa tatizo,” akasema Bw Kega.

Bw Chebukati hakunukuu kiasi cha fedha kinachohitajika kuthibitisha saini hizo.