Michezo

Washiriki wapya Super 8 watisha wakali wa soka

May 21st, 2019 2 min read

NA JOHN KIMWERE

KINYANG’ANYIRO cha kufukuzia taji la Super Eight Premier League (S8PL) msimu huu kinazidi kutetemesha huku washiriki wapya Githurai Allstars na Lebanon FC wakivuruga mahasimu wakuu.

Hata hivyo mabingwa watetezi, Jericho Allstars wanaendelea kutamba huku wakiongoza kwenye msimamo wa kipute.

Githurai Allstars kwa sasa imekamata nafasi ya pili kwa kuzoa alama 18, moja mbele ya Lebanon FC. “Tumepania kujituma kiume kwenye mkakati wa kuhakikisha mechi za tahidi kwa udi na uvumba kuhakikisha mechi za mkondo wa kwanza tumeibuka nafasi ya pili,” kocha wa Githurai Allstars, Fredrick Onyango alidokeza na kuongeza kuwa katika michezo ya mkumbo wa pili watakuwa mbioni kupigania kumaliza kileleni.

Aidha alidai kiasi wachezaji wake wameonekana kushindwa kuhimili makali ya wapinzani wao maana ndiyo mwanzo kushiriki kipute hicho. Katika mpango mzima anasema anaamini wamekaa pazuri kubeba taji la msimu huu.

Hata hivyo alikiri bayana kwamba ngarambe hiyo inashuhudia msisimko mkali hasa mbele ya wapinzani mabingwa watetezi, Jericho Allstars na Lebanon inayokuja kwa kasi msimu huu.

Githurai Allstars ilishangaza wengi iliposhinda mataji matatu mfululizo na kufuzu kushiriki kipute hicho.

Kwenye kampeni za Super Eight Daraja ya Kwanza mechi ya mwisho Githurai Allstars iliirarua Huruma Kona mabao 2-1 ambapo ilinasa tikiti ya kusonga mbele ilipoibuka kidedea kwa alama 79.

Nayo NYSA ni kati ya timu zilizokuwa miongoni mwa wapinzani wakuu msimu uliyopita, ambayo raundi hii kiasi imejikuta njia panda. Kocha wake, Fredrick ‘Oti’ Otieno anasema ”Tumekuwa na changamoto kadhaa ikiwamo suala ya utovu wa nidhamu miongoni mwa wachezaji wetu hali iliyochangia matokeo mabaya.”

Kocha huyo anadai kwamba ana imani tosha mambo yanakaribia kurejea kawaida maana wamelifanya suala hilo hasa kuwaweka kando wachezaji waliokiuka kanuni za klabu yao pia michezo.

Kwenye mechi za msimu uliyopita, NYSA ilikuwa kati ya vikosi vilivyotesa zaidi licha ya kuteleza na kushindwa kutwaa ubingwa huo uliobebwa na Jericho Allstars.

Naye kocha wa Jericho Allstars inayoongoza kipute hicho kwa alama 25, Thomas Okongo anasema wachezaji wake hawana lingine mbali wamepania kuendeleza ustadi wao wakilenga kuhifadhi taji hilo.

”Tumeweka pengo la pointi saba kati yetu na Githurai Allstars inayotufuata ambapo tuna imani ina kibarua kizito ili kutupiku,” alisema na kukiri kuwa bado kwenye kampeni hizo kamwe hakuna mteremko.

Kadhalika kampeni hizo zimeonekana siyo rahisi kwa kuzingatia Kawangware United ambayo ni mabingwa wa zamani msimu huu imejikuwa hoi. Kawangware United inavuta mkia kwenye orodha ya timu 16 kwa kuzoa alama saba pekee.