Habari Mseto

Washtakiwa kuhadaa watu watawatafutia ajira Kuwait

November 12th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYAKAZI watano wa maajenti wa kuwatafutia waliohitimu vyuo na taasisi za anuai kazi walishtakiwa Alhamisi kwa kuwalaghai watu tisa zaidi ya Sh1.2milioni wakidai watawatafutia kazi nchini Kuwait, mashariki ya kati.

Kevin Onyango Ogonde, Stellah Chemutai Chogwony, Habiba Ahmed Shaffia, Joseph Kagori Gikonyo na Franklin Otieno Okello walikanusha mashtaka 13 mbele ya hakimu mwandamizi Bw David Ndungi.

Watano hao walishtakiwa kutia vibindoni Sh1,234,500 kutoka kwa wasakaji kazi nchi za ughaibuni.

Mbali na shtaka hilo la pamoja Kevin alishtakiwa kumlaghai Justus Roche Opiyo Sh60,500 akidai atamsaidia kupata ajira Kuwait.

Chemutai alikana mashtaka manne ya kupokea jumla ya Sh225,000 kutoka kwa Charles Ngweno Omeda,James Ahoya,Antony Kinyua na Jeramiah Kamau akidai atawatafutia kazi Kuwait.

Habiba alishtakiwa peke yake kwamba alipokea kwa njia ya undanganyifu jumla ya Sh310,000 kutoka kwa  Ahoya, Simon Itagi Njuguna na Jeremiah Kamau akidai atawapeleka Kuwait.

Kagori alikana alimfuja Kennedy Njoroge Nduta Sh200,000 akimweleza atamtafutia ajira Kuwait.

Naye Okello alikana kumlaghai Waail Ahmed Sh100,000 kwa madai yay ohayo ya kuwatafutia ajira Kuwait.

Kesi itasikizwa Machi 21 2021. Waliachiliwa kwa dhamana mbali mbali kati ya Sh200,000 hadi Sh700,000 pesa tasilimu.