Habari Mseto

Washtakiwa kujifanya 'wamekwama' kimapenzi

April 15th, 2019 1 min read

NA CHARLES WANYORO

WATU watatu Jumatatu walifikishwa katika mahakama moja ya Meru kwa kujifanya kuwa wawili wao walikuwa ‘wamekwama’ baada ya kushiriki mapenzi, huku lengo lao kuu likiwa kujipatia pesa kutoka kwa wananchi.

Washtakiwa hao, waliotambuliwa kama Chacha Mwita, 24, Cynthia Makokha, 31 na Magoola Twaha, 27, walishshtakiwa kwa kupanga njama hiyo, huku lengo lao kuu likiwa kujipatIa fedha kutoka kwa umati uliokusanyika walimokuwa.

Inadaiwa walitoa kelele ili kuonyesha kuwa walikuwa ‘wamekwama’.

Mahakama iliambiwa kuwa walifanya kitendo hicho mnamo Jumapili katika chumba kimoja cha malazi katika eneo la Makutano, mjini Meru.

Bw Mwita na Bi Makokha walijifanya kuwa wamekwama, huku Bw Twaha akijifanya mganga aliyejaribu kuwatenganisha. Twaha ni Mganda.

Hata hivyo, walikanusha mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Maureen Odhiambo.

Waliachiliwa kwa dhamana ya Sh50,000 na mdhanini wa kiasi kama hicho ama dhamana ya Sh20,000 pesa taslimu. Kesi hiyo itasikizwa mnamo Mei 15.