Habari Mseto

Washtakiwa kuunda nakala feki za kandarasi za mamilioni

March 20th, 2018 1 min read

David Kahi Ambuku almaarufu Peter Bwonya Okwaro (kulia) na Paul Miller Owiti almaarufu Miller Nyami wakiwa kizimbani kwa kughushi kandarasi za ujenzi. Picha/RICHARD MUNGUTI

Na RICHARD MUNGUTI

WANAUME wawili walishtakiwa Jumatatu kwa kughushi kandarasi za Wizara ya Ujenzi.

Inadaiwa wawili hao katika afisi za wizara hiyo walilaghai watu kwa kuwapa kandarasi walizodai zimetiwa saini ya makatibu Profesa Paul Maringa Mwangi na Bi Nancy Karigithi.

Mabw David Kahi Ambuku almaarufu Peter Bwonya Okwaro na Paul Miller Owiti ajulikanaye kwa jina la msibo Miller Nyami walikanusha shtaka la kumlaghai Bi Mary Wanjiru Sh48.5milioni.

Washtakiwa kuwahadaa walioomba kandarasi hizi kwa kuwapa nakala walizodai zimetiwa saini na Bi Karigithi.

Baadhi ya waliolaghaiwa ni Bi Wanjiru, mkurugenzi wa kampuni ya Kinlix Limited. Walipokea kitita cha Sh48milioni wakidai watamuuzia vifaa vya kujenga barabara.

Okwaro na Nyami walikana mashtaka walipofikishwa mbele ya hakimu mkuu mahakama ya Milimani, Nairobi na kuachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh3 milioni.

Kesi itasikizwa Aprili 23.