Habari

Washtakiwa kwa kumpunja mfanyabiashara Sh2 milioni wakidai ardhi ina 'mapepo'

August 27th, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

WANAUME watatu wamefikishwa mahakamani jijini Nairobi ambapo wamekabiliwa na mashtaka ya kumhadaa na kumpunja Bw Harbans Singh Nandsingh Santa zaidi ya Sh2 milioni.

Inadaiwa watatu hao; Titus Fedha, Shariff Ali Haji, na Mzava Selemani Salum- na washukiwa wengine ambao hawakuwa mahakamani Jumanne – wameshtakiwa kwa kumpumbaza Bw┬áNandsingh Santa na hatimaye kumpunja zaidi ya Sh2 milioni kwa kudai vipande vyake viwili vya ardhi mtaani Westlands, nairobi alivyonuia kuviuza vilikuwa na mapepo yaliyohitaji kupungwa.

Mashtaka yanasema walimwambia mlalamishi kwamba wanafaa kuteketeza nyoka na vitu vingine vya ushirikina katika vipande hivyo vya ardhi kisha majivu kumiminwa katika Bahari Hindi.

Wanadaiwa kutekeleza makosa hayo kati ya Juni 10, 2019, na Julai 5, 2019.

Walikanusha mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh300,000 kila mmoja.

Kesi imepangwa kusikilizwa Septemba 26, 2019.