Habari Mseto

Washtakiwa ulaghai kwa dai ardhi ilikuwa na mapepo

August 28th, 2019 1 min read

Na SAM KIPLAGAT

WANAUME watatu ambao walimdanganya mfanyabiashara mmoja katika mtaa wa Kitisuru, Nairobi kwamba ardhi yake ilikuwa na pepo mbaya na uchawi ambapo ilihitaji kufanyiwa matambiko ili kutakaswa wameshtakiwa kwa ulaghai.

Washukiwa hao waliotambuliwa kama Mzava Selemani, Sharif Ali na Titus Fedha walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Milimani Francis Andayi kwa mashtaka ya njama za kumlaghai Harbans Singh Sh2 milioni.

Hata hivyo, wote walikana mashtaka hayo.

Walishtakiwa kuwa kati ya Juni 10 na 26 mwaka huu katika mkahawa wa Red Hill Garden katika mtaa wa Westlands, walipanga njama za kumlaghai mlalamishi Sh2 milioni kwa kumdanganya kwamba ardhi yake ambayo alipanga kuuza ilikuwa na pepo za kishetani.

Wanadaiwa kuwa na wengine ambao hawakuwa mahakamani.

Kulingana na mashtaka, walisema kuwa ardhi hiyo ilikuwa na nyoka na vifaa vingine vya kufanya uchawi ambapo nyoka alihitaji kuchomwa na majivu yake kurushwa katika Bara Hindi. Vifaa hivyo ni kama gamba la konokono, vibuyu na nguo.

Zaidi ya hayo, watatu hao walimlaghai Bw Harbhajan Singh na kupata Sh280,000. Inadaiwa walifanya kosa hilo kati ya Juni 24 na Julai 25 mwaka huu katika mtaa wa Kitisuru.

Kulingana na mashtaka, watatu hao na wengine ambao hawakuwa mahakamani walipanga njama za kumlaghai Bw Bhogal Sh280,000 kwa kudai kwamba ardhi yake ilikuwa na pepo za kishetani na ilipaswa kutakaswa.

Watatu hao waliagizwa kulipa dhamana ya Sh300,000 pesa taslimu ili kuachiliwa. Kesi hiyo itasikizwa mnamo Septemba 26.