Habari za Kaunti

Washukiwa 12 mbaroni kwa kupatikana na chang’aa

March 25th, 2024 1 min read

NA SAMMY KIMATU

WASHUKIWA 12 walikamatwa wakati wa msako dhidi ya pombe haramu na maduka ya kuuza vileo yasiyo na leseni mwishoni mwa juma.

Aidha, nyumba nne zilibomolewa na pombe aina ya chang’aa kutwaliwa na kuharibiwa.

Naibu kamishna Kaunti Ndogo ya Starehe, Bw John Kisang aliambia Taifa Dijitali kwamba operesheni hiyo iliongozwa na Msaidizi wa Kamishna tarafa ya South B, Bw Samuel Kimeu Ndambuki.

“Msako huo uliongozwa na Bw Kimeu akishirikiana na machifu, manaibu wa machifu na viongozi wa Nyumba Kumi mitaani. Walifanikiwa kukamata washukiwa 12 na tunatarajia watafunguliwa mashtaka na kufikishwa kortini leo (Jumatatu, Machi 25, 2024),” Bw Kisang akasema.

Msako huo ulifanyika maeneo ya Bellevue, Kituo cha biashara cha South B, Sana Sana, katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Fuata Nyayo sawa na kwenye maduka ya kuuza vileo kali na nyumba za kuishi zilizogeuzwa baa za kuuza pombe haramu.

“Kikosi changu kilivamia maduka 8 ya pombe ambayo yalifunguliwa kabla ya saa rasmi na yalikuwa yakifanya kazi bila leseni,” Bw Kisang alisema.

Watafunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Makadara.

Msimamizi huyo alikariri kuwa wakati wa operesheni, timu hiyo ilivamia na kuharibu nyumba 4 na kutwaa lita 15 za chang’aa.

Vilevile, alifafanua kwamba nyumba zilizobomolewa zilitumiwa kama maficho ya wahalifu.

“Nyumba nne za mabati zilizotumiwa kama klabu za kuuza pombe na maficho ya wakora pia hasikusazwa. Pombe nyingi aina ya chang’aa ilipatikana na kuharibiwa,” Bw Kisang akasema.

Milango yote na vifaa vingine kutoka kwa nyumba husika viliharibiwa.

Bw KIsang alionya kuwa msako zaidi unaendelea.

Naibu Rais, William Ruto anaongoza vita dhidi ya pombe haramu nchini na mihadarati, ambapo ameapa kutolegaza kamba.