Habari Mseto

Washukiwa 17 wa Al-Shabaab kusalia ndani

January 30th, 2019 2 min read

FADHILI FREDRICK na MOHAMED AHMED

MAAFISA wa kitengo cha kupambana na ugaidi (ATPU) kaunti ya Kwale wameruhusiwa na mahakama ya Kwale kuwazuilia vijana 17 wanaodaiwa kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la Al-Shabaab.?

Vijana ambao miongoni mwao ni wanawake wawili na wanaume 15, wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kushukiwa kuwa waduasi wa kundi hilo la kigaidi na ? kuwa na bidhaa bandia kinyume cha sheria.

Washukiwa hao ni pamoja na Nuru Sofia Alamini, Wilfred Mandisa Ngenge, Gerald Irungu Nyambura, Joseph Momanyi Obonyo, Albert Kilunga Abagaressa, Joseph Mrabu Charo, Daniel Safari Kadenga, Michael Muye Mwang’ombe, Christiano Krisha Daido na Abio Dadoo.

Wengine ni Christopher Najib Saro, Karisa Habel Randy, Kelvrin Ogongo Nyakundi, Robert Moreno Shaban, Isnino Fardia Hussein, Edwin Moroni na Collins Maina Mbogo.

Mahakama ya Kwale ilifahamishwa kwamba washukiwa hao walikamatwa Januari 28, 2019, Samburui ya eneobunge la Kinango, Kaunti ya Kwale.

Afisa wa polisi ambaye anaendeleza uchunguzi alisema washukiwa hao walipatikana kwenye vyumba viwili vya kukodisha.

Alisema wakati wa uvamizi huo, vijana hao walipatikana na bidhaa za matumizi ya jikoni zinazoaminika kuwa ghushi.

Pia walipatikana na simu za mkononi ambazo zinahitajika kufanyiwa ukaguzi zaidi ili kubainisha mawasiliano ya wandani wao.

Hata hivyo, wakiwa mbele ya Hakimu Mkuu, Bi Dominica Nyambu, walikana mashtaka hayo, wakisema wao ni wauza bidhaa za rejareja eneo la Samburu walioajiriwa na kampuni iliosajiliwa rasmi ya Primmax Marketing Limited yenye matawi yake sehemu mbalimbali eneo la Pwani.

“Washukiwa wanakabiliwa na makosa makubwa ya kiugaidi na ninaomba mahakama kuruhusu wazuiliwe kwa muda zaidi ili tubainishe ni kina nani na ni jinsi gani walivyoajiriwa ikizingatiwa ni vijana wanaotoka sehemu tofauti tofauti nchini,” akasema afisa anayeendeleza uchunguzi.

Baada ya kusomewa mashtaka yao baadhi ya washukiwa hao walieleza mahakama kuwa walinyanyaswa na maafisa wa usalama walipokuwa wanaendeleza operesheni yao.

Wengine walieleza kuwa hawana nia ya kujiunga na kundi hilo la kigaidi kwani kukusanyika kwao kulikuwa kwa sababu ya biashara waliyokuwa wameitiwa.

Baadhi ya waliokamatwa in pamoja na wale wanaosimamia shughuli za kampuni hiyo inayohusisha uuzaji wa bidhaa ndogo ndogo kama vile bakuli.

Akijitetea, mmoja wa washukiwa alisema kuwa hawezi kujiunga na kundi hilo kwani mamake mzazi ni miongoni mwa wale waliouawa katika shambulizi la kigaidi la Mpeketoni 2014.

Mahakama iliagiza washukiwa hao wazuiliwe kwa muda wa siku saba katika kituo cha polisi cha Diani huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Kesi hiyo itatajwa na kusikizwa Februari 4.

Washukiwa hao wamekamatwa takriban majuma mawili tangu Kenya iliposhuhudia tukio lingine la kigaidi katika hoteli ya Dusit, jijini Nairobi lililosababisha vifo vya watu 21.

Mashambulizi mengine ya kigaidi ambayo yamewahi kushuhudiwa nchini ni pamoja na la Westgate lililoua watu zaidi ya 67, na lile la Chuo Kikuu cha Garissa ambapo watu zaidi ya 144 waliangamia wengi wakiwa wanafunzi wa chuo hicho.

Serikali imeendeleza juhudi zake za kukabiliana na visa vya ugaidi hasa kufuatia tukio la hivi punde.