Habari za Kitaifa

Washukiwa 2 wa mauaji ya wanawake 42 Kware waachiliwa kwa dhamana


WASHUKIWA wawili wa mauaji ya wanawake 42 katika timbo la Kware, Embakasi, Nairobi wameachiliwa kwa dhamana ya Sh50, 000 kila mmoka, huku kibali cha kumtia nguvuni mshukiwa mkuu Collins Jumaisi kikitolewa.

Hakimu mkazi Irene Gichobi aliamuru Jumaisi aliyetoroka kutoka kituo cha Polisi cha Gigiri mnamo Agosti 20, 2024 akamatwe na kufikishwa kortini kushtakiwa kwa mauaji.

Bi Gichobi aliwaachilia huru Amos Momanyi na Moses Ogembo hadi Agosti 26, 2024 baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga kueleza korti “uchunguzi unaendelea na Jumaisi ametoroka.”

Lakini Bi Gichobi alifahamishwa kwamba DPP ameidhinisha Jumaisi ashtakiwe kwa mauaji.

“Baada ya kutathmini ushahidi katika faili sita zilizowasilishwa katika afisi ya DPP kusomwa, inabidi uchunguzi zaidi ufanywe kabla ya kushtaki washukiwa. Kwa sasa, wanaweza wakachiliwa kwa dhamana.”

Hata hivyo, mahakama ilielezwa kwamba DPP amesema kuna ushahidi wa kutosha kumshtaki Jumaisi kwa mauaji ya wanawake hao.

Idara ya usalama, hata hivyo, inasema ni wanawake 6 pekee waliouawa ila si idadi ya 42 inayotajwa.

Hakimu aliombwa atoe kibali cha kumkamata Jumaisi ambaye alitoroka seli za Kituo cha Polisi cha Gigiri, Nairobi.

Kufuatia kutoroka kwa Jumaisi, maafisa watano wa polisi walikamatwa na kufikishwa kortini, wakiwa ni; Koplo Ronald Babo, na makonstebo Evans Kipkirui, Zachary Nyabuto, Millicent Achieng na Gerald Mutuku.

Watano hao walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Martha Nanzushi na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh200, 000 kila mmoja.

Bi Nanzushi aliwaonya wasivuruge uchunguzi.

Jumaisi, Momanyi na Ogembo walitiwa nguvuni kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya wanawake hao ambao miili yao iliyokuwa imekatwakatwa na kuwekwa ndani ya magunia na kutupwa ndani ya timbo la Kware, eneo la Embakasi, Nairobi.

Bi Gichobi aliwaruhusu polisi kuwazuia kwa siku saba zaidi mnamo Agosti 16, 2024.

Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 26, 2024 kwa maagizo zaidi.

Polisi walisema wanataka kukamilisha uchunguzi dhidi ya watatu hao.

Bi Gichobi Munamo mnamo Agosti 16, 2024 alikubalia ombi la Inspekta Patrick Wachira kuendelea kuwahoji Collins Jumaisi, Amos Momanyi na Moses Ogembo hadi Jumatatu, Agosti 26, 2024.

Bi Gichobi alifahamishwa na Inspekta Wachira kwamba polisi wamekamilisha uchunguzi wa mauaji ya wahasiriwa sita ambao maiti zao zimetambuliwa na watu wa familia.

“Tayari tumekamilisha uchunguzi wa wahasiriwa sita ambao jamaa zao wamefaulu kutuambua miili yao katika chumba cha Maiti cha City,” Inspekta Wachira alimweleza hakimu.

Afisa huyo aliomba polisi wapewe siku 21 zaidi kuwawezesha kukamilisha uchunguzi katika mauaji hayo ya kutatanisha.

Maiti za wahasiriwa hao ziliguduliwa zimekatwakatwa vipande na kupakiwa ndani ya magunia na kutupwa ndani ya timbo la Kware.

Akiwasilisha ombi la kupewa muda zaidi, Inspekta Wachira alisema polisi wanaendelea kusubiri utambuzi wa miili inayohifadhiwa katika chumba cha maiti cha City.

Mchunguzi huyo wa jinai alieleza mahakama kuwa polisi wamependekeza washukiwa hao watatu washtakiwe kwa mauaji ya wanawake hao sita.

Wananchi walisaidiana na polisi kuzoa maiti zilizokuwa zimewekwa kwenye magunia, na kupelekwa mochari.

Mawakili wanaotetea washukiwa wa unyama huo, waliomba mahakama itie kikomo uchunguzi kwa kuamuru mashtaka yawasilishwe dhidi ya washukiwa hao.

Awali, mawakili hao walieleza Mahakama kwamba haki za washukiwa hao zimeendelea kukandamizwa ikitiliwa maanani kwamba walikamatwa Julai 2024 na wangali mikononi mwa polisi.

Hakimu aliamuru washukiwa hao Collins Jumaisi, Amos Momanyi na Moses Ogembo wanaodaiwa kuhusika na mauaji hayo yaliyotamausha wengi, wasalie ndani hadi Agosti 26, 2024 watakapoelezwa ikiwa watashtakiwa kwa mauaji au la.

Jumaisi, hata hivyo, alitoroka kutoka seli za kituo cha Polisi Gigiri mnamo Agosti 20.

Washukiwa wenza wawili wameachiliwa kwa dhamana ya Sh50, 000, kila mmoja.

Polisi waliwakamata washukiwa hao baada ya simu za baadhi ya wanawake hao waliofariki kupatikana na mmoja wao.