Habari Mseto

Washukiwa 43 wa ugaidi kukaa kizuizini siku 2

January 23rd, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA 43 wa ugaidi waliokamatwa siku mbili zilizopita watazuiliwa katika makao makuu ya Polisi wa Kupambana na Ugaidi (ATPU) ili kuhojiwa kuhusu uhusiano wao na magaidi wa Al Shabaab.

Hakimu mwandamizi, Bi Zainab Abdul alisema Polisi wanahitaji kupewa muda kubaini iwapo washukiwa hao wana uhusiano wowote na kundi la kigaidi la Al Shabaab.

Mahakama ilipunguza muda wa wiki moja ambao polisi waliomba hadi siku mbili.

Washukiwa hao walikamatwa mnamo Junuari 21,2020 katika Chuo cha Alison & Atlas kilichoko mtaani Eastleigh Nairobi. Wakurugenzi wa chuo hicho ni Bi Asha Ali Sarat na Ali Yusuf Ali.

Asha na Ali watashtakiwa kwa kumiliki chuo bila kukisajili katika wizara ya Elimu chini ya idara ya TVET na bila leseni.

Mameneja wanne waliokamatwa pamoja na wakurugenzi hao ni Nasra Noor Ibrahim, Omar Muhumed Yahya, Mohamed Issa Mohamed na Edward Odinga Mulumba.

Akiamuru washukiwa hao miongoni mwao mvulana wa miaka 14, Bi Abdul alisema “lazima polisi wapewe muda wa kutosha kusaka uhalali wa hati zilizopatikana na washukiwa”.

Hakimu huyo alikubali ombi la Inspekta Richard Ngatia kutoka idara ya ATPU lililotaka washukiwa wazuiliwe na kuhojiwa.

“Ijapokuwa Polisi waliomba muda wa siku tano, mahakama hii itawaruhusu wawazuilie washukiwa kwa muda wa siku mbili tu,” alisema hakimu.

Hakimu huyo alisema lazima haki za washukiwa pamoja na maslahi mengine ya umma yatiliwe maanani ndipo “ haki itendeke.”

Hakimu alisema mawasilisho ya Inspekta Ngatia yaliegemea mno kuhusu hati za usafiri , vitambulisho na vifaa vya mawasiliano ambavyo polisi walitwaa kutoka kwa washukiwa walipowatia nguvuni Januari 21, 2020.

“Mahakama hii inakubaliana na wakili Shadrack Wambui kwamba polisi hawahitaji kukaa na washukiwa hao kubaini wakati paspoti, vitambulisho, vifaa vya elektroniki vikikaguliwa,” alisema Bi Abdul.

Hakimu alisema licha ya tetezi zote za wakili huyo kupinga washukiwa kuzuiliwa, polisi wanahitaji kupewa fursa ya kuhakikisha iwapo washukiwa hao wana uhusiano wowote na magaidi wa Al Shabaab au la.