Habari Mseto

Washukiwa 5 wa ugaidi wanaswa wakila njama

January 20th, 2020 2 min read

LEONARD ONYANGO na KALUME KAZUNGU

WASHUKIWA watano wa ugaidi walikamatwa wikendi wakidaiwa kuchunguza eneo la burudani jijini Nairobi kwa lengo la kutekeleza shambulio.

Washukiwa hao walinaswa Jumamosi na maafisa wa Kitengo cha Kukabiliana na Ugaidi (ATPU), wakikagua eneo la Whiskey River Lounge katika Barabara ya Kiambu. Walikuwa wakikagua eneo hilo kwa kutumia gari dogo jeupe, kulingana na polisi.

Wanajumuisha Mohamed Hassan Bario (raia wa Somalia), Mohamed Adan (dereva Mkenya), Hodan Abdi Ismail (raia wa Somalia), Ifrah Mohammed Abshir (raia wa Somalia) na Mohamed Abas Mohamud ambaye ni raia wa Amerika.

Walizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Pangani na wanatarajiwa kufikishwa mahakamani leo.

Polisi walisema washukiwa hao walipatikana na suruali ambayo ni sare ya wanajeshi wanahewa, tisheti na kofia ya kijeshi.

“Kadhalika, washukiwa hao walipatikana na fedha zilizojumuisha sarafu ya Kenya na dola ya Amerika, kipakatakilishi, paspoti ya Amerika, hundi na kitambulisho cha maafisa wa usalama wanaolinda ubalozi wa Amerika,” ikasema taarifa ya polisi.

“Picha za gari walilokuwa wameabiri zilisambazwa katika vituo vyote na baadaye likanaswa katika eneo la Pangani,” ikaongezea.

Huku hayo yakijiri, maafisa wa usalama katika Kaunti ya Lamu, jana walifanikiwa kutibua shambulio la kigaidi katika eneo la Pandanguo, Witu, baada ya kuwalemea magaidi zaidi ya 50 wa Al-Shabaab waliokuwa na silaha hatari.

Makabiliano baina ya polisi na magaidi hao yalidumu kwa muda wa saa tano kuanzia saa nne na nusu usiku, Jumamosi.

Mzee wa Kijiji cha Pandanguo Adan Golja, aliambia Taifa Leo kuwa magaidi hao walifika kijijini hapo saa nne usiku.

Inadaiwa kuwa magaidi hao waliwahoji baadhi ya wakazi kuhusu hali ya usalama katika eneo hilo.

“Baada ya kufahamishwa kuwa eneo hili lilikuwa likilindwa na maafisa wa GSU na wanajeshi wa KDF, magaidi hao walionekana kuingiwa na hofu. Hapo ndipo walisema kuwa hawakuwa katika eneo hilo kuzua vurugu bali kuvuna mahindi,” akasema Bw Golja.

Mmoja wa wakazi waliohojiwa na magaidi hao waliripoti kwa Bw Golja ambaye aliwafahamisha polisi wa akiba.

Kulikuwa na ufyatulianaji wa risasi baina ya magaidi hao na maafisa wa polisi wa akiba. Dakika chache baadaye maafisa wa GSU na KDF waliwasili katika eneo hilo.

“Mapigano kati ya maafisa wa usalama na magaidi yalianza nne na nusu usiku 1Jumamosi hadi saa tisa alfajiri, Jumapili. Magaidi hao walilemewa lakini walivuna mahindi yote katika shamba la ukubwa wa ekari moja na kisha kuingia mafichoni katika Msitu wa Boni,” akaelezea Bw Golja.

Kamishna wa Kaunti, Bw Irungu Macharia alithibitisha tukio lakini akasema hali ya utulivu imerejea.