Habari Mseto

Washukiwa 6 wa bunge la Nairobi waachiliwa ili wafanyakazi walipwe

August 28th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WAFANYAKAZI sita wakuu katika bunge la kaunti ya Nairobi walishtakiwa Jumatatu kwa kuruhusu kampuni ya mmoja wao kulipwa Sh0.9 millioni kwa njia ya ufisadi.

Punde tu wafanyakazi hao walipokukanusha mashtaka dhidi yao mahakama iliambiwa huenda wafanyakazi wa bunge la kaunti hawatapokea mishahara kwa vile mmoja wa washukiwa hao ndiye anayeruhusu malipo.

“Nataka kuifahamisha hii mahakama kuwa kushtakiwa kwa Bw Jacob Ngwele Muvengei kutaathiri malipo ya mishahara kwa vile ndiye amepewa idhini ya kutumia mtandao wa Ifmis peke yake.

Yeye ndiye Karani wa Bunge la Kaunti na kisheria ndiye huwalipa mishahara wafanyakazi wengine wote. Kuzuiliwa kwake bila shaka kutaathiri malipo ya mishahara na huduma nyinginezo za kifedha,” wakili Nicholas Kamwende alifichua kortini.

Hakimu mwandamizi Bw Lawrence Mugambi aliombwa amawachilie Bw Muvengei kwa dhamana na kumruhusu afike katika afisi za bunge kuidhinisha malipo.

“Kumzuilia Bw Muvengei kwa siku nyingi kutavuruga malipo ya mishahara ikitiliwa maananji ni mwisho wa mwezi,” Bw Kamwende alimjulisha hakimu.

Ili kuokoa hali ya suintofahamu ya utendakazi katika bunge hilo, Bw Mugambo aliwaachilia wafanyakazi hao kwa dhamana ya Sh500,000 pesa tasilimu kila mmoja na kuitaka bunge hilo iandikie barua mahakama iwakubalie washtakiwa kufika kortini baada ya kuidhinisha malipo ya mihahara ya wafanyakazi.

Pia Bw Mugambi aliwataka wafanyakazi hao waandamane na afisa wa polisi kutembelea afisi za bunge hilo aidha kuchukua hati muhimu ama kuidhinisha utenda kazi uendeleaa.

Mbali na kulipa dhamana hiyo kila mmoja alitakiwa awasilishe  pasi yake ya kusafiria mahamani na wale hawana wawasilishe barua kutoka kwa idara ya Uhamiaji ikieleza hawajawahi pewa cheti cha kusafiri.

“Ikiwa washtakiwa hawa wataendelea kuzuiliwa wafanyakazi katika bunge hili la kaunti ya Nairobi kukosa kulipwa mishahara. Mshtakiwa wa kwanza Bw Muvengei ndiye Karani mkuu wa Bunge hili. Ndiye anayekubaliwa kuruhusu malipo ya mishahara ya wafanyakazi wote wa bunge hili,” wakili Nicholas Kamwende alimjulisha hakimu.

Wakili huyu alisema hayo baada ya Mabw Muvengei,  Adah Awuor Anyango, James Kariuki Kaguma, Raphael Mwinzi Maluki , Fredick Macharia Mwani na Bi Philomena Kavinya Nzuki kushtakiwa kwa ufisadi.

Wote sita walishtakiwa kwa kufanya njama za kuifilisi bunge la kaunti hiyo kwa kuruhusu kampuni ya Primara Ventures Sh997,950 pasi kuwasilisha vitabu kwa kituo cha bunge hilo.

Bw Maluki alishtakiwa kupokea pesa hizi kupitia akaunti yake iliyoko Benki ya Equity mnamp Julao 5 2017 akidai kampuni yake ya Primara Venture ilikuwa imeuzuia bunge la kaunti vitabu vya kutumia katika kituo chake cha urtenda kazi.

Wote sita walikabiliwa na shtaka la kuidhinisha kampuni ya Primara kupokea malipo wakijua haikuwa imewasilisha vitabu.

Bw Muvengei alikabiliwa na shtaka la kutofuata sheria kwa kuruhusu malipo ya maelfu hayo ya pesa.

Bi Onyango ambaye ni naibu wa Bw Muvengei alishtakiwa kwa kutumia mamlaka yake vibaya kwa kuruhusu malipo hayo.

Bi Nzuki ambaye ni Mhasibu mkuu wa Bunge na mkaguzi alishtakiwa kuruhusu malipo kwa kampuni ya Primara klinyume cha sheria.

Bw Kaguma , ambaye ni afisa mkuu wa ununuzi alishtakiwa kwa kuamuru naibu wake Bi Daisy Mueni Muema kurodhesha makampuni matano kuwania ununuzi wa vitabu vya kituo cha bunge hilo kinyume cha sheria.

Bw Mwangi ameshtakiwa kwa kudai amepokea vitabu hivyo kutoka kwa kampuni ya Primara.

Bw Muvengei na Bi Nzuki walishtakiwa pamoja kulipa Primara pesa za vitabu kwa njia ya ufisadi.

Kesi itatajwa Septemba 11.