Washukiwa 9 wa wizi wa mabavu watoroka seli za polisi Thika

Washukiwa 9 wa wizi wa mabavu watoroka seli za polisi Thika

NA LAWRENCE ONGARO

WASHUKIWA tisa wa wizi wa mabavu waliozuiliwa kwenye seli za kituo cha polisi cha Thika, walitoroka na msako umeanzishwa dhidi yao.

Kamanda mkuu wa polisi katika kanda ya Kati, Bw Manasse Musyoka, alithibitisha kuwa washukiwa hao tisa walitoroka kutoka kwenye seli za polisi Thika.

Hata hivyo alisema mmoja wao anaendelea kuzuiliwa na polisi kwa mahojiano baada ya kunaswa akiruka ukuta wa seli ili atoroke.

Ilidaiwa ya kwamba mnamo Jumatano usiku mwendo wa saa nne za usiku mmoja wa washukiwa hao alitaka kwenda haja naye polisi aliyekuwa kazini akafika kufungua lango ili waandamane naye.

Katika hali hiyo washukiwa hao walifurika pamoja langoni na kutafuta mbinu ya kutoka huku wakipanda ukuta na kuruka upande wa nje ya seli za polisi.

Polisi huyo aliyekuwa peke yake mahali hapo alitafuta usaidizi kutoka kwa maafisa wenzake ambao walianza msako mkali ili kuwanasa washukiwa hao, huku wakinasa mmoja wao.

Washukiwa hao tisa ni Livingstone Mwangi Njau, Francis Mwangi Matheri, Allan Njogu Mungai, Charles Nyaga Mitatu, John Mbugua Murege, Eric Ngigi musige, Arthur Ndung’u Kavemba, Vinton Kaguku Mbugua, na Joseph Githu Nyaguthii ambaye alitiwa nguvuni akijaribu kutoka.

Kamanda mkuu wa polisi Bw Musyoka, amesema kuwa uchunguzi tayari umeanza ambapo polisi wote waliokuwa kazini usiku huo watasaidia maafisa wa upelelezi wa DCI na uchunguzi.

Washukiwa hao wanakabiliwa na makosa mazito ya wizi wa mabavu ambapo iwapo watanaswa watashtakiwa kwa makosa ya kutoka kwenye seli za polisi.

Alitoa wito kwa wananchi popote walipo kusaidia polisi kwa kuwataja washukiwa hao iwapo wangeweza kuwatambua.

“Tukiwapata washukiwa hao itakuwa ni afueni kwetu kwa sababu wakiwa huru ni hatari kwa usalama wa umma,” alifafanua kamanda huyo.

  • Tags

You can share this post!

ICC yamruhusu wakili Gicheru kutumia ushahidi

Ruto anamtaja naibu leo naye Raila ni kesho

T L