Habari Mseto

Washukiwa motoni kwa kuchafua kuta za seli kwa kinyesi ili wasifikishwe kortini

October 23rd, 2018 1 min read

ONYANGO K’ONYANGO na EDITH CHEPNGENO

KISANGA kilizuka Jumatatu katika kituo cha polisi cha Central mjini Eldoret baadhi ya washukiwa waliokamatwa Jumapili walipochafua seli kwa kinyesi ili wasipelekwe kortini.

Shughuli katika kituo hicho zilikwama kwa saa kadha baada ya washukiwa kuchafua kuta na sakafu ya seli kwa kinyesi.

Washukiwa hao zaidi ya 20 walipaswa kupelekwa kortini jana asubuhi lakini maafisa katika kituo hicho hawakuweza kuvumilia uvundo kutoka ndani ya seli.

Iliripotiwa kuwa ni washukiwa watatu walioenda haja kubwa ndani ya seli na kutumia kinyesi kuchafua kuta.

Kulingana na mkuu wa idara ya kuzima moto Kaunti ya Uasin Gishu, Bw Peter Kurgat, idara yake iliitwa kusafisha uchafu huo hali ilipobadilika kuwa mbaya zaidi.

“Kwa sababu ya ushirikiano wetu wa kikazi na polisi, tuliitwa kusafisha seli baada ya washukiwa kuamua kuichafua kwa kinyesi. Walikuwa wamechafua kuta zilizo karibu na eneo la kupokea wageni lakini tumesafisha. Niliambiwa kwamba hawakutaka kupelekwa kortini,” Bw Kurgat aliambia Taifa Leo.

Baadaye, polisi walifaulu kuwapeleka washukiwa hao kortini.