Habari za Kaunti

Washukiwa sita wakamatwa kwa kuteketeza bangi, kusaidia mlanguzi kutoroka

January 27th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

POLISI katika Kaunti ya Murang’a wametia mbaroni washukiwa sita ambao inadaiwa waliteketeza bangi ya thamani ya Sh300,000 na pia wakamsaidia mlanguzi wa shehena hiyo kutoroka mnamo Januari 24, 2024.

Washukiwa hao wanaaminika kwamba walikuwa wateja wa bangi hiyo na wakati maafisa wa polisi walifika kumkamata mlanguzi na pia mihadarati hiyo, washukiwa hao wakazua purukshani.

Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa kaunti ndogo ya Kigumo Kiprono Tanui, operesheni hiyo ya Jumamosi asubuhi ilikuwa ya kusaka washukiwa ambao walitibua juhudi za kumkamata mlanguzi pamoja na bangi yake katika kijiji cha Rwanyambo.

Kisa hicho kiliishia maafisa wa polisi waliokuwa wameweka mtego wa kumnasa mlanguzi huyo sugu  kurejea katika stesheni yao ya Muthithi wakiwa mikono mitupu, hali ikiishia kazi bure.

“Maafisa wangu walikuwa wametekeleza busara na ustadi kufuatilia mienendo ya mlanguzi sugu ambaye hushirikisha biashara hiyo yake katika mitaa ya Kaharate, Heho, Maragua na Sabasaba. Walipata habari za ujasusi kwamba alikuwa apokezwe shehena ya kilo 20 ya bangi na pia misokoto 370,” akasema Bw Tanui.

Hata hivyo, wakati maafisa hao walijitokeza ghafla katika harakati za mlanguzi huyo kukagua shehena hiyo katika kichaka kimoja cha kijiji hicho cha Rwanyambo, nao wateja waliokuwa wakitegea kujinunulia bangi hiyo walijitokeza na kuzua purukshani.

“Katika hali ya mshikemshike iliyotokea, mlanguzi alihepa pamoja na wanaume wawili waliokuwa wakimsaidia kutekeleza uhalifu huo. Aidha, polisi walipokuwa katika harakati za kujaribu kuwasakama washukiwa hao wasitoweke, wateja nao waliiwasha bangi hiyo moto na wengine wakijinyakulia ya bure na kuhepa nayo mbio,” akasema.

Bw Tanui alisema kwamba kile kilichonaswa ni pikipiki mbili ambazo zinaaminika kuwa za kushirikisha biashara hiyo ya mihadarati.

“Maafisa walizitwaa pikipiki hizo na tungetaka anayezimiliki ajitokeze katika kituo cha polisi cha Muthithi ili kuzitambua na pia kutupa stakabadhi zake za umiliki ndio pia atuelezee zilikuwa zikifanya nini katika kikao cha bangi,” akasema.

Bw Tanui alilalamika kwamba operesheni hiyo ilitibuliwa na waraibu wa bangi “ambao ndio tunajaribu kuokoa kupitia misako ya kuwazima walanguzi”.

Alisema kisa hicho kinatia maafisa wa polisi wasiwasi kwamba “tunajaribu kuokoa watu ambao tayari wamejipa imani kwamba bangi kwao ni nzuri na haifai kukamatwa”.

Hata hivyo, aliapa kuendelea mbele na misako hiyo “na hata kwa sasa mlanguzi huyo kwa kuwa tunamjua bado tunamsaka na wakati wowote tutamtia mbaroni”.

Bw Tanui alisema kwamba “mlanguzi huyu ako na makesi kadha katika mahakama za Kenol na Kigumo na ambapo huwa anaachiliwa kwa bodi licha ya kwamba amethibitisha kwamba hana nia ya kukoma kuvunja sheria”.

Bw Tanui aliteta kwamba “kazi yetu imekuwa ya kumsifikiza hadi mahakamni kumshtaki lakini naye huwa anatusidikiza kurudi kwa stesheni akiwa ameachiliwa huru kwa dahamana rahisi”.

Alisema washukiwa hao sita watashtakiwa kwa makosa ya kuzuia polisi wafanye kazi yao, kumsaidia mshukiwa kuhepa na pia uharibifu wa ushahidi.

[email protected]