Habari

Washukiwa wa al-Shabaab washambulia basi la kuelekea Lamu, waua watu watatu

January 2nd, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

WASHUKIWA wa al-Shabaab wameshambulia basi la kuelekea Lamu eneo la Nyongoro katika Kaunti ya Lamu, ambapo wameua watu watatu huku idadi sawa na hiyo wakiachwa na majeraha.

Wahanga alikuwa ni utingo na abiria wawili wa basi la kampuni ya Simba Coach.

Basi la ‘Mombasa Raha’ lilishambuliwa mwanzo kwa kumiminiwa risasi lakini dereva akafululiza kwa kasi na hivyo kunusurika.

Tukio hilo la kutamausha limethibitishwa na Kamishna wa Kaunti ya Lamu Bw Irungu Macharia.

“Ni kweli. Ripoti zilizonifikia ni kwamba watu watatu wameuawa huku wengine watatu wakijeruhiwa vibaya. Wapiganaji wamevamia basi la kampuni ya Mombasa Raha lililokuwa limetoka Mombasa kuelekea Lamu na kulimiminia risasi. Maafisa wetu tayari wamefika kwenye eneo la tukio kuwasaka wahalifu hao waliotorokea kwenye msitu wa karibu. Usafiri kwenye barabara ya Lamu-Garsen pia tumeusitisha kwa muda. Shughuli zitarejelewa baadaye. Watu wasiwe na shaka,” amesema Bw Macharia.

Shambulio hilo la Alhamisi asubuhi limetekelezwa dhidi ya basi hilo lililokuwa linasafirisha abiria kutoka Mombasa.

Hii ni baada ya awali kuwa ameahidi kutoa maelezo muhimu.

“Ninaelekea eneo la mkasa, lakini tayari ninawasiliana na maafisa walioko katika eneo la tukio,” Bw Macharia alikuwa ameambia ‘Taifa Leo’ mapema kwa simu.

Usafiri katika barabara ya Lamu-Garsen umesitishwa mnamo wakati ambapo vyombo vya usalama wakiwemo wanajeshi wamedhibiti hali baada ya unyama huo kutendeka.

Baadaye Alhamisi wanajeshi wa KDF wamefanikiwa kuwaua washukiwa wanne wa al-Shabaab na wakamkamata mmoja baada ya shambulio la basi Lamu; haya yamethibitishwa na Mshirikishi wa eneo la Pwani, John Elungata.

Katika miezi ya karibuni wanachama wa al-Shabaab – kundi lenye makao yake Somalia – wamekuwa wakitekeleza mashambulizi katika miezi ya majuzi.

Mnamo Jumamosi, Desemba 28, 2019, shambulio dhidi ya basi lilisababisha vifo vya makumi ya watu katika eneo la shughuli nyingi jijini Mogadishu.

Idadi ya walioangamia ilizidi watu 70.

Katika eneo la Kotulo, Kenya, watu 10 walipoteza maisha yao baada ya wapiganaji kushambulia basi wakitumia kilipuzi wiki moja iliyopita.

Wapiganaji wa kundi hilo pia walitekeleza shambulio Desemba 26, 2019, eneo la Liboi ambapo waliwateka nyara wafanyabiashara wawili baina ya mpaka wa Kenya-Somalia. Waliwaachilia baadaye Desemba 27, polisi wakisema walikuwa wameanzisha msako kuwakamata waliohusika.