Habari Mseto

Washukiwa wa biashara chafu ya pesa wanaswa Ruiru

October 24th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

POLISI wa mjini wa Ruiru wamewanasa washukiwa saba wanaohusika na biashara ya fedha bandia pamoja na makosa ya utakatishaji fedha.

Afisa mkuu wa polisi katika Kaunti ya Kiambu, Bw Ali Nuno, alisema kwamba Jumanne usiku, maafisa wake walinasa washukiwa watatu kutoka eneo la Githurai wakiwa na sarafukadha za Euro.

Alieleza kuwa kiasi cha sarafu zilizonaswa ni noti 8,890 za Euro sawa na kiasi cha pesa za Kenya Sh102,236,000 milioni.

Zilinaswa kwenye sefu moja pamoja na vifaa vya kutengeneza pesa za bandia.

“Kwa muda mrefu kumekuwa na wizi na uhalifu mwingine wa fedha kwenye benki za hapa mjini Ruiru lakini tunawapongeza wananchi kwa kuwaarifa polisi kuhusu washukiwa hao watatu,” alisema Bw Nuno.

Wanawake watatu

Alisema polisi walivamia jumba moja eneo la Githurai saa tisa alfajiri mnamo Jumanne ambapo wanawake watatu walitiwa nguvuni.

Wakati huo huo pia washukiwa wanne mjini Ruiru walinaswa kwenye chumba cha ATM cha Barclays Bank tawi la Ruiru, wakijaribu kuiba fedha.

Hata hivyo, kabla ya kutekeleza wizi huo, maafisa wa polisi waliwanasa mara moja na kuwapeleka kituoni kwa mahojiano zaidi.

Ni kutokana na juhudi za wananchi waliowashuku ambao walilazimika kuwajulisha polisi waliofika hapo mara moja.

Washukiwa hao walikuwa ni mlinzi mmoja wa KK Guard wa Nairobi, wawili kutoka G for S na mhudumu mmoja wa biashara ya uchukuzi ya bodaboda.

“Washukiwa hao wataendelea kuhojiwa zaidi katika kituo cha polisi cha Ruiru huku wakingoja kufikishwa mahakamani wakati wowote,” alisema mkuu huyo wa polisi.

Alisema kuna uwezekano wa walinzi wa benki kuwa na ufahamu wa namba ya kodi ya kutoa fedha hizo.

Afisa huyo alieleza kuwa Oktoba 3, 2019, kulikuwa na jaribio lingine la wizi wa pesa katika Family Bank mjini Ruiru.

Alisema maafisa wa upelezi wako katika harakati ya kuchunguza kwa kina ni jambo lipi linalosababisha wizi wa benki kuongezeka mjini Ruiru.

Alisema wizi wa kuiba kwenye benki umeongezeka sana ambapo polisi wanalazimika kutumia ujuzi mwingi wa kukabiliana nao.

Alidokeza pia kuwa kwa wiki mbili zilizopita mshukiwa mmoja eneo la Juja alinaswa na kadi 1000 za Sim Card za Safaricom na alifikishwa mahakamani baada ya kuhojiwa.

Alisema teknolojia inavyoendelea kuimarika ndivyo chanzo cha hali ya wizi wa benki kuzidi kushuhudiwa katika kila sehemu nchini.