Habari Mseto

Washukiwa wa mauaji ya mwanamke wakamatwa wakipokea matibabu

January 4th, 2024 1 min read

NA SAMMY KIMATU

MAKACHERO wanachuguza kisa ambapo mwili wa mawanamke ulipatikana ndani ya nyumba katika jumba la Papino lililoko South B katika kaunti ndogo ya Starehe usiku wa kuamkia Alhamisi.

Naibu mkuu wa polisi katika eneo la Makadara Dennis Omuko alisema kufuatia tukio hilo, washukiwa wawili walikamatwa walipokuwa wakisaka matibabu katika hospitali ya Mbagathi.

Bw Omuko alisema waliokamatwa ni pamoja na aliyedaiwa kuwa rafiki wa marehemu na mwenzake kwa jina John Matara,34, na Anthony Nyongesa,25, mtawalia.

Polisi walipata kisu kilichokuwa na damu, shuka za kitanda zikiwa na damu, mipira ya kondomu, chupa ya pombe, simu aina ya Samsung, kibeti na pasipoti ya marehemu aliyetambuliwa na polisi kwa jina Bi Starlet Wahu Mwangi, 26.

“Mwili wa marehemu ulikuwa sebuleni huku ukiwa umelala kifudifudi na alama za kudungwa kwa kisu kichwani na kwenye paja. Kulikuwa na alama kadhaa za majeraha mengine mwilini huku damu nyingi ikitapakaa katika chumba hicho. Mwili huo haukuwa umevalishwa nguo,” Bw Omuko akasema.

Washukiwa walizuiliwa katika seli za kituo cha polisi cha Industrial Area.