Habari Mseto

Washukiwa wa shambulizi la DusitD2 ndani siku 30

January 23rd, 2019 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA watano wa ugaidi miongoni mwao raia wa Canada waliamriwa Ijumaa wazuiliwe kwa muda wa siku 30 kuhusiana na shambulizi la Hoteli ya Dusit D2 ambapo watu 21 waliuawa Jumanne.

Hakimu mwandamizi Bi Martha Mutuku alikubalia ombi la Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kwamba washukiwa hao wazuiliwe kuwasaidia polisi kuwatambua washirika wa magaidi watano waliotekeleza uhalifu huo.

Kupitia kwa viongozi wa mashtaka Mabw Duncan Ondimu na Eddy Kadebe , DPP alisema polisi wanahitaji muda wa kuwahoji washukiwa hao watano waliokamatwa baada ya shambulizi hilo la hoteli hiyo.

Mabw Ondimu na Kadebe walieleza korti kuwa washukiwa hao Guled Abdihakimu (raia wa Canada) , madereva wa teksi Joel Ng’ang’a Wainaina na Oliver Kanyango Muthee , muhudumu wa Mpesa Gladys Kaari Justus na mmiliki wa duka la Supa Bw Osman Ibrahim wanatuhumiwa walikuwa na ushirikiano kwa njia moja au jigine na magaidi hao walioshambulia hotelui hiyo mwendo was aa tisa mchana.

Hakimu mwandamizi Martha Mutuku. Picha/ Richard Munguti

Mahakama iliambiwa shambulizi hilo liliendelea kwa siku mbili Januari 15 na 16, 2019.

Korti ilijulishwa kuwa madereva hao wa teksi walikuwa wanawapeleka magaidi hao mahala tofauti tofauti jijini.

Polisi wanachunguza akaunti zao kwa lengo la kuona matumizi yao na pesa walizokuwa wanapokea.

Gladys ambaye ni mihudumu wa Mpesa anahojiwa kuhusiana na viwango vya pesa alizokuwa anatuma kwa watu mbali mbali.

“Uchunguzi umebaini mmoja wa magaidi waliouawa Ali Salim Gachunge alikuwa akiishi katika mtaa wa Muchatha eneo la Ruaka kaunti ya Kiambu na mshukiwa sugu wa ugaidi Bi Violet Kemunto Omwoyo,” alisema Bw Ondimu.

Kiongozi wa mashtaka Eddy Kadebe, washukiwa watano wa ugaidi kutoka kulia Joel Ng’ang’a Wainaina, Oliver Kanyango Muthee, Gladys Kaari Justus, Guled Abdihakim na Osman Ibrahim. Picha/ Richard Munguti

Bi Omwoyo anayesakwa na polisi alikuwa amenunua simu nne za rununu na kila wakti alikuwa anawasiliana na washukiwa wa kundi la Alshaabab nchini Somalia.

Mahakama ilielezwa Gachunge aliyeuawa katika shambulizi hilo la Dusit alikuwa na simu tatu za rununu na simu za washukiwa hao watano zimetwaliwa kufanyiwa uchunguzi na maafisa wa idara ya uhalifu wa mitandao.

Mahakama ilijuzwa kwamba washukiwa hao wanachunguzwa kwa makosa ya kuwapa hifadhi magaidi , kuwasaidia magaidi kutekeleza uhalifu na kuwa wanachama wa makundi ya ugaidi.

“Adhabu ya makosa hayo ni vifungo vya miaka 20 na 30,” alisema Bw Ondimu huku akiomba “ Polisi wapewe muda zaidi.”

Mahakama ilielezwa magaidi hao walienda kwenye hoteli hiyo na gari nambari KCN 340E na mle ndani kuliokotwa simu mbili muundo wa Techno na Nokia ambayo haikuwa na simukadi.

“Inaaminika washukiwa hawa watano wakp na uhusiano na magaidi waliomo nchini na ng’ambo,” alisema Bw Ondimu.

Hussein Muhumed. Picha/ Richard Munguti

Korti ilijulishwa magaidi waliotekeleza shambulizi hilo wako na washirika wenzao nchini na “ mahojiano na washukiwa hawa watano yatawaumbua magaidi hawa sugu.”

Mahakama iliombwa itilie maanani mashambulizi ya kigaidi ambayo yameteekelezwa siku za hivi punde.

Bw Wainaina aliyetiwa nguvuni karibu na hospitali ya MP Shah atahojiwa kuhusu safari zake za kila mara katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Polisi watachunguza akaunti zake na pia magari mengine yake kubaini jukumu alililotekeleza.

Pia polisi watachunguza idadi ya simu zilizopigwa na washukiwa hao watano ndipo wajulikane waliokuwa wakiwasiliana nao.

Bi Mutuku alikubalia ombi la DPP na kuamuru washukiwa hao “ wazuiliwe hadi Feburuari 18 2019 kuwasaidia polisi kukamilisha uchunguzi.”

Na wakati huo huo mshukiwa mwingine Hussein Muhumed alitiwa nguvuni mjini Mandera Janauri 18 (Ijumaa) aliamriwa pia azuiliwe.

Mahakama ilifahamishwa kuwa Bw Muhumed anachunguzwa kubaini uhusiano wake na washukiwa wa ugaidi.

Mahakama ilielezwa alikutwa akiwa na vitambulisho vya Kenya na Uganda mjini Mandera.