Kimataifa

Washukiwa wa ubakaji waachiliwa, korti yasema sura ya mlalamishi haivutii

March 12th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

WANAUME wawili waliachiliwa huru na mahakama ya Italia kwa makosa ya kumbaka mwanamke, baada ya majaji kuamua kuwa mdhulumiwa ana ‘uanaume wa kimaumbile’ na hivyo hangevutia mbakaji.

Wawili hao, ambao wote ni wa miaka 22 waliachiliwa mnamo 2017, lakini sababu ya kuachiliwa kwao ilielezwa Machi, wiki iliyopita, wakati mahakama ya rufaa iliamrisha washtakiwe tena.

Majaji walisema kuwa washtakiwa walibaini kuwa mwathiriwa hakuwa na maumbile ya kuvutia, kwani hata mmoja wao aliandika namba yake ya simu kuwa ya ‘Viking’ kuashiria kuwa maumbile yake hayakuvutia.

Mamia ya raia Jumatatu walikongamana nje ya mahakama hiyo Ancona na kuandamana kuhusu uamuzi huo wa majaji.

Waandamanaji hao zaidi ya 200 waliilaumu mahakama kuwa na mapendeleo.

Washukiwa walishtakiwa mnamo 2016 kwa kosa la kumbaka mwanamke mnamo 2015, lakini korti ikatupilia mbali mashtaka hayo, ikisema maelezo ya mdhulumiwa hayakuwa ya kuaminika.

Mwanamke huyo alikuwa amedai kuwa alibakwa na mwanamume wakati mwenzake alikuwa akitazama, baada yao kumwekea dawa katika kinywaji.

Madaktari walisema majeraha yake yalionyesha kuwa alibakwa na kuwa damu yake ilipatikana na chembechembe za dawa.

Lakini majaji waliamua kuwa “haingewezekana kuwapo kwa uwezekano kuwa ilikuwa mdaiwa wa kudhulumiwa” ndiye alipanga mkutano baina yao jioni hiyo kama ilivyoripotiwa.

Walisema kuwa “mwanamume anayetuhumiwa kumbaka hata hakumpenda msichana, kwani hata alinakili nambari yake ya simu kwa jina la utani ‘viking’ kuashiria angekuwa kitu chochote, wala si mwanamke, ila kiumbe cha dume.”

“Picha iliyo katika faili yake ilithibitisha hili,” akasema Jaji.

Kesi hiyo itasikizwa tena upya na mahakama nyingine ya Perugia katika tarehe itakayoamuliwa.