Habari Mseto

Washukiwa wa ufisadi warushwe rumande kesi zikiendelea – Wabukala

October 18th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) sasa inataka washukiwa wa ufisadi wawe wakisukumwa rumande kesi zao zinapoendelea kusikizwa.

Hata hivyo, msimamo huu wa Mwenyekiti wa tume hiyo, Askofu Mkuu (Mstaafu) Eliud Wabukala ni kinyume cha Katiba, ambayo katika vifungu vya 49 na 50 inasema kila mshukiwa ana haki ya kupewa dhamana, isipokuwa pale kuna sababu kubwa za kufanya azuiliwe kesi ikiendelea.

Askofu Wabukhala alisema kuzuiliwa kwa washukiwa kutasaidia katika vita dhidi ya ufisadi ili kuepusha ufujaji wa mabilioni ya pesa za umma.

Idadi kubwa ya washukiwa wa ufisadi ambao wameshtakiwa wako nje kwa dhamana kesi zao zikiendelea kusikizwa.

“Hivi majuzi, Jaji Mkuu aliahidi kuhakikisha kesi za ufisadi zinaharakishwa. EACC itazidi kuunga mkono msimamo huo na hata kuomba kuwe na maagizo ya kuweka washukiwa ndani wakati kesi zinapowasilishwa mahakamani,” akasema.

Alikuwa akizungumza jana katika hafla ya kuzindua rasmi Taasisi ya Kitaifa ya Mafunzo ya Uadilifu (NICA) jijini Nairobi.

Taasisi hiyo itakuwa ikitoa mafunzo kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wa sekta ya kibinafsi kuhusu masuala ya uadilifu, mbinu za kupambana na ufisadi, usimamizi bora, uongozi bora miongoni mwa masuala mengine.

Askofu Wabukala alikariri hatua zilizopigwa na tume hiyo katika kupambana na ufisadi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, akisema hawatalegeza kamba na watazidi kushirikiana na asasi nyingine kumaliza uozo huo.

Katika kipindi hicho, EACC iliripoti kuzima wizi wa Sh4.2 bilioni za umma na ikitambua mali 14 ya umma iliyokuwa imenyakuliwa na watu binafsi inayokadiriwa kuwa za thamani ya Sh2.3 bilioni. Alisema tayari mali ya thamani ya Sh352 milioni imerudishwa mikononi mwa umma.

Tume hiyo pia ilikamilisha uchunguzi wa visa 183 vya ufisadi na kuwasilisha faili hizo kwa Idara ya Mashtaka ya Umma, ambapo ilipendekezwa visa 135 vifunguliwe mashtaka, na 14 vichukuliwe hatua za kinidhamu katika mashirika ambako washukiwa wanahudumu.

Bw Wabukhala jana alisema kwa sasa, kuna zaidi ya visa 3,000 vya ufisadi vinavyochunguzwa na EACC ambavyo vinahusu maafisa wa ngazi za juu katika serikali ya kitaifa na za kaunti.

“Tunachukulia kwa uzito zaidi kesi zinazohusu maafisa walio na mamlaka ya juu na pia zile zinazohusu wizi wa kiasi kikubwa cha pesa. Tunafahamu kila Mkenya anataka kuona wahusika wa ufisadi wakiadhibiwa kwa hivyo tutaharakisha kasi kuwasilisha faili zetu za uchunguzi kwa DPP, ambaye tunashirikiana naye katika juhudi hizi,” akasema.

Alionya watumishi wa umma waamue kama wanataka kuendelea kutumikia wananchi kwani hakutakuwa na mazingara ya kuendeleza ufisadi na wanaotaka kujitajirisha kwa kufuja pesa za umma ni heri wajiuzulu.

Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC, Bw Halakhe Waqo, na Katibu wa Wizara ya Elimu anayesimamia ustawishaji wa mafunzo ya kitaaluma, Bw Alfred Cheruiyot miongoni mwa wengine.