Habari za Kitaifa

Washukiwa wa uvamizi wa shamba Naivasha wazuiliwa Nairobi

March 5th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA 21 akiwamo mwanaharakati Bernard Macharia Mwangi, wamezuiliwa katika kituo cha polisi cha Lang’ata kwa kuvamia shamba linalohusishwa na Rais William Ruto na kuharibu ua wa thamani ya Sh2.8 milioni.

Bw Mwangi, James Maina Makena, Ruth Wangui Mwangi, David Mwaura Wanjiru, Eliud Kinyanjui Mungai, John Maina Ngugi, Julius Kinyua John, Elijah Mugwe Ndenderu na Hiram Ngatia Ndirangu waliamriwa wasalie ndani hadi Machi 6, 2024, watakaporudishwa kortini.

Wengine waliofikishwa katika mahakama ya Milimani ni Alvin Kamano Ngugi, Ann Wanjiku, Daniel Njogu Njuguna, George Kimani Thuku, Paul Maina, Benjamin Ndirangu Mwangi, James Ngugi Nganga na Joseph Macharia Mwaura.?

Hakimu mwandamizi Gilbert Shikwe aliombwa na kiongozi wa mashtaka Judy Koech aamuru washukiwa hao kuzuiliwa kwa siku 14 kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi kubaini kiini cha washukiwa hao kuvamia shamba hilo linalomilikiwa na kampuni ya Eburru Hills Farm Limited, inayohusishwa na Rais Ruto.

Bi Koech alisema washukiwa hao walitiwa nguvuni baada ya Meneja wa Eburru kuwasilisha ripoti kwamba washukiwa hao walivamia shamba hilo na kuharibu ua wa thamani ya Sh2.8 milioni.

“Naomba washukiwa hawa wazuiliwe kwa siku 14 kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi na kuandikisha taarifa za  mashahidi,” alisema Konstebo Nelson Ratemo.

Mahakama ilielezwa imebidi washukiwa hawa washughulikiwe Nairobi kukwepa taharuki.

Afisa huyo alisema kufuatia kutiwa nguvuni kwa Mbw Mwangi na Makena, vitisho vilizuka vya kuvamia kituo cha polisi cha Naivasha kwa nia ya kuwaokoa.

“Kulikuwa na vitisho vya kuvamia kituo cha polisi cha Naivasha kuwanusuru washukiwa hawa. Ililazimu wasafirishwe hadi Nairobi,” Bw Ratemo alimweleza Bw Shikwe.

Lakini ombi la kuwasafirisha washukiwa kutoka Naivasha hadi Nairobi lilipingwa vikali na wakili Mbugua Mureithi aliyeeleza mahakama kwamba polisi wanakandamiza haki za washukiwa hao.

“Hakuna mtu aliyehatarisha maisha ya washukiwa. Huu ni uvumi tu wa polisi kujaribu kuonyesha kuna hatari inayowakabili washukiwa kwa lengo la kutaka kuwadhulumu,” alisema Bw Mureithi.

Wakili huyo alisema polisi walipeleka kesi hiyo katika mahakama ya Kajiado ikakataliwa huku wakielezwa “inafaa kusikilizwa katika mahakama ya Naivasha ambako ndiko shamba liko.”

Mahakama ilifahamishwa kwamba polisi wamekaidi Kifungu 36 cha Katiba kinachowapa wananchi uhuru wa kutangamana.

Bw Mureithi alichacha kwamba kuwasafirisha washukiwa kutoka Naivasha hadi Nairobi ni njia ya “kuwafanya wakimbizi wa ndani kana kwamba hawana kwao.”

Bw Mureithi aliomba washukiwa waachiliwe kwa dhamana na kuwataka waripoti kwa Bw Ratemo ikiwa kuna haja.

Bw Shikwe atatoa uamuzi Machi 6, 2024.