Habari za Kaunti

Washukiwa wa wizi, ufunguaji simu za M-Kopa wanyakwa Mpeketoni

June 6th, 2024 2 min read

NA KALUME KAZUNGU

POLISI Mpeketoni katika Kaunti ya Lamu wamewakamata washukiwa wanne wa wizi na ufunguaji wa simu za M-Kopa.

Wanne hao ni wanaume watatu na mwanamke mmoja. Walinyakwa kwenye maduka tofauti tofauti mjini Mpeketoni, ambapo jumla ya simu 76, zikiwemo za kawaida na zile za M-Kopa, vipakatalishi na vifaa vingine vinavyowasaidia kutekelezea ujanja na wizi huo, vilipatikana.

Ripoti ya polisi mnamo Jumatano iliwatambua wanne hao kuwa ni Paul Kinyua Katiuki na Sidi Joice Shida waliopatikana na simu 46 ambapo 13 kati ya hizo, ni za M-Kopa.

Walinaswa kwenye duka la fundi wa kukarabati kompyuta kwa jina Dan Computerized Repair Shop.

Pia walipatikana na vifaa vingine vya kuwasaidia kutekelezea wizi.

Mshukiwa wa tatu aliyenaswa ni Eliud Ng’ang’a,42, aliyekamatwa akiwa kwenye duka la kielektroniki la High-Tech Electronics Repair.

Bw Ng’ang’a alipatikana na simu 13 ambazo inaaminika ni za wizi, pamoja na vifaa mbalimbali vya kiufundi vya kumsaidia kutekelezea ujanja.

Wa nne aliyekamatwa ni John Mutembei,24.

Bw Mutembei alinaswa kwenye duka la fundi wa kukarabati simu la JM Phones Repair, ambapo simu 17 zinazojumuisha tisa za M-Kopa zilipatikana.

Pia kompyuta mbili na kifaa cha kuhifadhia data vilipatikana.

Baadhi ya simu na kompyuta ambazo polisi na maafisa wa M-Kopa walipata kutoka kwa washukiwa. PICHA | HISANI

Washukiwa hao wa wizi walinaswa baada ya polisi kutekeleza msako wa kushtukiza kwenye mji huo unaovuma kibiashara.

Soma Pia: Ushindani mkali wa kibiashara wainua mji wa Mpeketoni

Mji huo uko Lamu Magharibi.

Msako wa maafisa hao wa polisi pia ulitekelezwa kufuatia malalamishi ya muda mrefu na shinikizo za wananchi kufuatia kukithiri kwa visa vya wizi, hasa ule wa simu za M-Kopa kwenye mji huo wa Mpeketoni na viunga vyake.

“Jumatano majira ya saa saba, maafisa wetu kutoka kituo cha polisi cha Mpeketoni, wakiandamana na maafisa wa kushughulikia maswala ya simu za M-Kopa na wafanyakazi wao, walifanya msako na kuwanasa washukiwa wa wizi na utapeli. Hii ni baada ya kupokea taarifa za kijasusi kutoka kwa umma kuhusu wizi uliokuwa ukiendelea na ujanja wa kufungua simu,” ikasema ripoti hiyo ya polisi.

Wanne hao wanazuiliwa kwenye kituo cha polisi cha mjini Mpeketoni huku msako na uchunguzi zaidi ukiendelea.

Kunaswa kwa wanne hao kumepokelewa kwa furaha na baadhi ya wakazi na wenyeji wa Mpeketoni.

Bi Alice Kamau ambaye amewahi kuibiwa simu na vifaa vingine dukani mwake, aliwasihi polisi kuendeleza misako zaidi, akisema washukiwa zaidi bado wanatawala eneo hilo na kuendeleza uovu wao.

“Nimefurahi kusikia kuna washukiwa wa wizi walionaswa na polisi. Wizi wa simu, hasa ni donda sugu hapa mjini Mpeketoni. Naona ni mwamko mpya kwa polisi wetu kuanzisha misako na kuwanasa washukiwa,” akasema Bi Kamau.

Naye Bw Joseph Waweru alielezea matumaini yake kwamba misako hiyo ya mara kwa mara ya polisi dhidi ya wezi Mpeketoni itasaidia kumaliza visa vya wizi na utukutu eneo hilo.