Habari Mseto

Washukiwa waliodunga OCS kwa mishale akisaka wapishi wa chang’aa watambuliwa

April 1st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI 

WAKAZI wa kijiji cha Gachororo, Juja ambapo Msimamizi wa Kituo cha Polisi (OCS) alivamiwa mnamo Jumapili usiku, Machi 31, 2024 akiendeleza oparesheni dhidi ya pombe haramu na hatari, wamefichua washukiwa wa shambulizi hilo.

Bw John Misoi, afisa mwenye cheo cha Inspekta na ambaye ni OCS, alishambuliwa kwa kudungwa mishale wakati akiongoza polisi kukabiliana na kero ya chang’aa.

Siku moja baada ya kisa hicho, washukiwa wa shambulio hilo wametambuliwa kama ‘Theuri’ na ‘Kioni’.

Kwa mujibu wa sheria za Idara ya Polisi (NPS), ni hatia kushambulia afisa wa polisi hasa akiwa na sare rasmi wakati akitekeleza majukumu yake Kikatiba.

Aidha, hatua hiyo inafasiriwa kama njia kujiepushia lawama – msako mkali ukitarajiwa kufanyika kutia nguvuni wahusika.

Katika barua ya wakazi wa kijiji hicho ambapo Inspekta Misoi alidungwa kwa mishale, wameambia Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki kwamba muuzaji sugu wa chang’aa eneo hilo anajulikana kama Theuri.

Kwenye barua hiyo wazi, wenyeji hao kupitia mshirikishi wao Bw James Thuira walisema kwamba “inajulikana vyema kwamba Bw Theuri akisaidiana na Bw Kioni ndio hunogesha biashara ya chang’aa na bangi miongoni mwa wanakijiji hao”.

Huku maafisa wa polisi nao wakijazana mitandaoni kutangaza kisasi dhidi ya shambulizi lililomwacha mkubwa wao akipambania uhai katika hospitali moja Mjini Thika, wakazi waliomba wasichukuliwe kama washirika wa wakora hao.

“Ukweli ni kwamba Bw Misoi alifika na maafisa wake katika nyumba ya Bw Theuri na walipobisha, mshukiwa huyo aling’oa dirisha la nyumba yake na akahepa,” wenyeji wanasema kupitia barua hiyo.

Aidha, wanasema kwamba Bw Misoi alikuwa amesimama nje ya nyumba ya mshukiwa.

“Bw Theuri alihepa huku akipiga makelele kwamba amevamiwa na wakora na ndipo majirani walianza kupiga nduru,” barua yao inaelezea.

Ni katika harakati hizo ambapo kutoka gizani Bw Misoi alishambuliwa kwa mishale, akaanguka chini akiwa na majeraha naye akipiga nduru za maumivu.

“Maafisa waliokuwa ndani ya nyumba ya Theuri walitoka nje na wakakimbiza mkubwa wao hadi hospitali ambapo anaendelea kutibiwa,” barua ya wakazi inaongeza.

Sasa kijiji cha Gachororo kinasemwa kuwa katika hali ya taharuki kukitarajiwa msako mkali kumaliza biashara ya pombe haramu na mihadarati na pia wa kusaka washukiwa walioshambulia afisa wa polisi.

Naibu Rais, Rigathi Gachagua ametangaza vita kali dhidi ya pombe haramu na hatari, ambapo msako unaendelea kote nchini.