Washukiwa wanne wakamatwa kwa kudaiwa kuiba nyaya za stima eneo la viwanda, kaunti ya Nairobi

Washukiwa wanne wakamatwa kwa kudaiwa kuiba nyaya za stima eneo la viwanda, kaunti ya Nairobi

Na SAMMY KIMATU

NAIROBI

WASHUKIWA wanne walikamatwa usiku ewa kuamkia jana na polisi wakidaiwa kuiba nyaya za stima katika eneo la Viwanda, Kaunti ya Nairobi.

Mkuu wa polisi eneo la Makadara, Bw Timon Odingo alisema wanne hao ni wanaume kutoka eneo la Kambi Moto mtaani wa mabanda wa Mukuru-Kaiyaba. Aidha, Bw Odingo aliambia Taifa Leo washukiwa walipatikana wakichimbua na kukata nyaya za stima kwa lengo la kuuza kwa wanunuzi wa vyuma kuu kuu.

Isitoshe, kwa mujibu wa kamanda Odingo, washukiwa walipojaribu wakati mmoja kukata nyaya hizo, sauti ya mlipuko na cheche za stima zilisikika na kuwavutia polisi waliokuwa wakishika doria. Kisa hiki kilitokea mkabala wa barabara ya Busia karibu na mtaa wa Kayaba.

“Wanaume hao walipokuwa wakikata stima, mlipuko mkubwa ulisikika kabla ya stima kutoa spaki. Maafisa wa usalama waliokuwa wakishika doria karibu na barabara ya Busia walifika haraka na kuwaamrisha kujisalimisha mara moja,” Bw Odingo akaeleza.

Polisi walitwaa baadhi ya vifaa vilivyotumika kutekeleza uhalifu kutoka kwa washukiwa. Vilevile, washukiwa, kwa mujibu wa polisi ni miongoni mwa genge linalosakwa kwa udi na uvumba kufuatia uunganishaji wa stima kutoka kwa trasfoma, taa za barabarani na kutoka kwa Viwanda.

“Wakiiba stima huwa wanasabazia wakazi mtaani kwa kati ya Sh500 na Sh1,000 kwa matumizi ya nyumbani na kazini mtawalia,” Bw Odingo akanena. Seikali imekaza kamba kuwakamata watu wanaounganisha stima kinyume cha sheria na kuuzia wananchi huku kampuni ya Kenya Power ikipoteza mabilioni ya pesa kila mwaka kupitia wizi wa stima na trasfoma.

You can share this post!

Twaha Mbarak kuwania urais FKF

Lempurkel aomba aachiliwe kwa dhamana kabla ya kesi...

T L