Habari Mseto

Washukiwa watano wa mauaji ya polisi wakamatwa Lamu

June 10th, 2020 1 min read

Na KALUME KAZUNGU

WASHUKIWA watano wametiwa mbaroni kuhusiana na mauaji ya afisa wa polisi katika kijiji cha Tchundwa, Kaunti ya Lamu Jumatatu usiku.

Rodgers Odhiambo ambaye ni afisa wa polisi wa cheo cha konstebo aliyekuwa akihudumu kwenye kituo kidogo cha polisi cha Tchundwa, alikumbana na mauti yake pale genge la watu watatu waliojihami kwa mapanga, visu na marungu lilipomvamia muda mfupi baada ya kuondoka kituoni.

Imebainika kuwa, Bw Odhiambo aliondoka kituoni baada ya kupigiwa simu na mmoja wa marafiki zake ambaye ni raia aliyemtaka wakutane kijijini hapo.

Akithibitisha kukamatwa kwa watano hao, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Irungu Macharia amesema operesheni kali ya kuwanasa washukiwa zaidi inaendelea eneo hilo.

Amesema waliokamatwa watasaidia maafisa kutekeleza uchunguzi na kuhakikisha washukiwa halisi wa mauaji hayo ya Jumatatu wanabainika na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Kwa sasa tumewakamata washukiwa watano wa mauaji ya afisa na miongoni mwao ni rafiki ya afisa huyo aliyempigia simu ili wakutane kabla ya afisa kuuawa. Pia tumewatia mbaroni wamiliki wa nyumba ambapo afisa huyo aliuawa,” amesema Bw Macharia.

Wakati huo huo, kamishna huyo ametoa onyo kali kwa wakazi ambao wamekuwa wakijihami kwa visu na mapanga kwenye maeneo ya umma, akisema polisi wako macho na watawatia mbaroni watu kama hao.

Amesema hivi majuzi vijana wapatao 40 waliokuwa wamejihami walikamatwa Tchundwa, Myabogi na Mbwajumwali wakati wa operesheni kali ya kuwasaka wahalifu wa mapanga na visu.

Mnamo 2015 idara ya usalama, Kaunti ya Lamu ilipiga marufuku kwa wakazi dhidi ya kujihami kwa visu na mapanga maeneo ya umma.

“Marufuku bado yapo na yeyote tutakayempata akiwa amejihami kwa upanga, kisu au rungu kwenye maeneo ya umma tutamkamata,” amesema Bw Macharia.