Habari za Kaunti

Washukiwa watano wakamatwa Mukuru, maafisa waharibu lita 341 za pombe haramu

March 7th, 2024 2 min read

NA SAMMY KIMATU

WASHUKIWA watano wamekamatwa Alhamisi kwenye msako ulioendeshwa asubuhi dhidi ya pombe haramu.

Akithibitisha, Naibu Kamishna wa Kkaunti ndogo ya Starehe John Kisang aliambia Taifa Leo kwamba operesheni hiyo ilifanyika katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Maasai katika tarafa ya South B.

Watu watano walikamatwa huku nyumba saba zilizotumiwa kama vilabu vya kuuzia pombe hiyo zikibomolewa.

Lita 310 za pombe aina ya Toibo na lita 31 za pombe haramu ya chang’aa zilinaswa na vifaa vilivyotumika kutengeneza pombe hiyo vikitwaliwa na kisha kuharibiwa.

Bw Kisang aliongeza kwamba operesheni hiyo iliongozwa na mkuu wa tarafa ya South B Solomon Muranguri akishirikiana na chifu Paul Muoki Mulinge, manaibu wa chifu na viongozi wa mitaa.

Aliongeza kwamba nia ya msako huo ni kupambana kumaliza vileo haramu ambavyo vinasababisha wanaume na hasa vijana kuzembea, ni hatari kwa maisha ya wanaotumia na pia pombe hiyo huuzwa bila leseni na ni aina ya vileo ambavyo serikali ilipiga marufuku.

“Tunaendeleza operesheni zetu kote katika kaunti ndogo ya Starehe. Serikali kupitia kwa naibu wa rais, Rigathi Gachagua imetuagiza tushirikiane na wasimamizi wa tabaka mbalimbali ili kuhakikisha hakuna pombe inayoweza kudhuru watu na haina leseni inastahili kuuziwa wananchi. Pia, tuna maagizo ya kumaliza maficho yote yanayotumiwa na wahalifu hasa kwenye manyumba pombe ya aina hii zinakopatikana mitaani,” Bw Kisang akasema.

Vilevile, aliwaonya wafanyabiashara wanaoendesha uuzaji wa pombe haramu ndani ya nyumba kwamba wanavunja sheria na nyumba zote za aina hiyo zitabomolewa.

Aliongeza kwamba wakibomoa nyumba husika, mabati, miti na milango hutumiwa katika makao ya watoto na miti kutolewa kama kuni kupikia wanafunzi chakula shuleni.

Katika kukurukakara za operesheni hiyo, watu wengi walijipata katika partashika ambayo hawajaizoea kwani wengine walikuwa wangali usingizini msako huo ukianaza.

“Nilikuwa nimelala lakini nikashtuka na kuamka niliposikia milango na mabati yaking’olewa kumbe baadaye nikabaini kulikuwa na msako wa maafisa wa utawala wakisaka pombe haramu katika mtaa wa Maasai Village,” mama anayeuza mboga mtaani huo akasimulia.

Wapitanjia waliorauka saa kumi na mbili asubuhi walipata fursa ya kutazama sinema ya bwerere huku baadhi ya wateja wakiwa katika hali ya kila mmoja wao mguu niponye.

“Wanaume wengine wanaozoea kunywa asubuhi maarufu ‘kutoa lock’ kabla ya kuelekea katika maeneo wanakofanya kazi walilazimkika kuingia ndani ya mtio Ngong ili wasikamatwe,” Bw Daniel Musyimi akaeleza.

Bw Kisang amehapa kuendeleza misako hiyo kote mitaani.

[email protected]