Habari

Washukiwa wawili wa ugaidi kukaa ndani siku 10 uchunguzi ukamilike

January 8th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA wawili wa ugaidi Jumanne walitiwa ndani kwa siku 10 wakichunguzwa zaidi ambapo wanatuhumiwa kupiga picha kituo cha maafisa wa polisi wa haiba ya juu kilichoko Ruiru.

Wawili hao James Mburu Ikaba na Miriam Njoki, mahakama ilikubali wazuiliwe katika makao makuu ya polisi wa kupambana na ugaidi ATPU.

Hakimu mwandamizi katika mahakama ya Milimani, Nairobi Bw Kennedy Cheruiyot ndiye alitoa uamuzi huo.

Bw Cheruiyot alikubali ombi hilo liliwasilishwa na afisa wa ATPU Sajini Geofrey Busolo.

“Nakubali ombi la Polisi kwamba washukiwa hawa wawili; Ikaba na Njoki wazuiliwe kwa siku 10 kuhojiwa na kufanikisha ushahidi,” alisema Bw Cheruiyot.

Ikaba na Njoki walitiwa nguvuni Jumatatu mjini Ruiru wakituhumiwa kupiga picha kituo hicho cha GSU Recce Company kilichoko Ruiru.

Akiwasilisha ombi la kuzuiliwa kwa washukiwa hao, Sajini Busolo aliambia mahakama wawili hao walikuwa ndani ya gari aina ya Land Cruiser iliyokuwa imeegeshwa karibu na kituo hicho cha GSU.

Walikuwa wakikichukua chukua picha na pamoja na maeneo yanayokizunguka.

Baada ya kuwaona maafisa wa GSU, Mburu aliyekuwa anaendesha gari hilo alijaribu kuchomoka mbio lakini akatiwa nguvuni.

Polisi waliokuwa wanawaandama wawili hao walipiga risasi magurudumu ya gari hilo ndipo ikasimama.

Polisi waliwapeleka washukiwa hao katika kituo cha polisi cha Juja ambapo walihojiwa.

Polisi walipata raundi saba za risasi na baadaye wakampeleka Mburu nyumbani kwake mtaani Marurui, Ruiru ambapo walipata vitu kadhaa miongoni mwavyo bastola muundo wa Ceska, bunduki na raundi 45 za risasi.

Washukiwa hao walipelekwa kituo cha ATPU Nairobi na baada ya kuhojiwa wakakiri walikuwa wanafanya uchunguzi na kupokea taarifa muhimu.

Bw Busolo alisema wawili hao watafunguliwa mashtaka ya kufanya uchunguzi wa asasi ya Serikali kinyume cha sheria za ugaidi za 2012.

Wakipatikana na hatia watasukumwa jela miaka 20.

Aliomba washukiwa hao wazuiliwe kwa siku 10 kwa sababu wakiachiliwa watatoroka.