Washukiwa wawili wakamatwa kwa kuiba paipu za maji

Washukiwa wawili wakamatwa kwa kuiba paipu za maji

Na SAMMY KIMATU

NAIROBI

WASHUKIWA wawili walikamatwa mwishoni mwa wiki kwa kudaiwa kuharibu mradi wa maji uliofadhiliwa na Benki la Dunia katika mtaa mmoja wa mabanda kaunti ya Nairobi.

Akiongea na Taifa Leo jana, mkuu wa polisi eneo la Makadara, Bw Timon Odingo alithibitisha washukiwa hao walikamatwa katika mtaa wa mabanda wa Kayaba, kaunti ndogo ya Starehe. Aidha, Bw Odingo aliongeza kwamba washukiwa walipatikana wamechimbua mchanga, wakakata na kuiba paipu za chuma zilizowekwa kusambaza maji mitaani kuuza kama vyuma kuukuu.

Fauka ya hayo, Bw Odingo alieleza kwamba washukiwa waliokamatwa watawasaidia wapelelezi kufanikisha kuwakamata washukiwa wengine wanaoaminiwa kushirikiana katika sakata hiyo.

“Wanaume wawili walipatikana na maafisa wa polisi mtaani Kayaba wakikata paipu za maji na wamekuwa wakiviuza kwa wafanyabiashara wanaonunua vyuma vilivyotumika. Watatusaidia kuwakamata wenzao wanaoshirikiana katika uhalifu huo,” Bw Odingo akanena.

Kwa mujibu wa polisi, washukiwa wamekuwa wakichimbua vyuma hivyo nyakati za usiku na kuvikata vipande vidogo vifupi kisha kuzipeleka kupima wakiuzia watu wanaonunua vyuma vilivyotumika. Polisi waliongeza kuwa kila paipu moja ina uzito wa kilo 120 na kwa kila kilo wanauza Sh50 bei ya mtaani.

Vilevile, mdokezi wetu aliyekuwa mfanyakazi katika mradi huo wa maji mtaani humo alisema paipu zilizowekwa katika mitaa ya Mukuru ni za urefu unaotoshana sawa na kilomita 16. “Tuliweka paipu zote mitaani ya Mukuru ambazo ni sawa na umbali wa kilomita 16. Kila paipu moja ina uzito wa kilo 120,” Mdokezi akasema.

Mradi huo ulinuiwa kuwasaidia wakazi katika mitaa ya Mukuru kupata maji safi kwa bei nafuu ili kuwapa afueni badala ya kuhangaika kwa uhaba wa maji kwa muda mrefu. “Serikali ilikuwa na nia ya kusambaza maji masafi na yenye bei nafuu kwa wakazi mitaani ya Mukuru ili kupunguza walaghai wanaowatoza wakazi ada ya juu.

Kila mtungi mmoja wa lita 20 za maji ulinuiwa kuuzwa Senti 50,” Ofisa mmoja wa utawala mtaani South B akanena. Vilevile, paipu zote ni za chuma kizito na zimewekwa mtaani wa mabanda wa Kayaba, Maasai, Hazina, Sokoni, Fuata Nyayo, Kenya Wine na Kisii Village.

Baada ya watu wasiojilikana kuiba paipu za maji katika mradi wa Benki kuu ya Dunia, mradi wenyewe umekwama huku mamilioni ya pesa yakitumika kwa minajili ya kuwasaidia wakazi mitaani ya mabanda kaunti ya Nairobi.

You can share this post!

Xavi Hernandez arithi mikoba ya Koeman kwa kishindo

Pigo Pogba akijiondoa katika kikosi kwa jeraha

T L