Habari MsetoVideo

Washukiwa wengine 3 wakodolea macho kifo

May 16th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

WASHUKIWA saba wanaoshtakiwa kwa kumtwanga na kumpora kimabavu mfanyabiashara Timothy Muriuki  Sh100,000 wanakondolea macho adhabu ya kifo wakipatikana na hatia.

Wanashtakiwa chini ya kifungu cha sheria nambari 296 (2) za uhalifu na adhabu yake huwa ni  kifo ama hakimu akiwaonea huruma awafunge kifungo cha maisha.

Kufikishwa mahakamani kwa Mabw Benjamin Peter Mulinge, Bernard Onyango Otieno na Michael Banya Wathigo kumefikisha saba idadi ya washukiwa walioshtakiwa kwa shambulizi hilo miongoni mwao Bw Muriuki akiwamo Mbunge anayewakilisha Kenya katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) Bw Simon Mbugua.

Watatu hao walikanusha mbele ya hakimu mkuu Bw Francis Andayi kuwa walimnyang’anya Bw Muriuki Sh100,000 na kumwumiza wakati wa kisa hicho.

Mnamo Jumanne mshukiwa wa nne Bw Brian Shem Owino alishtakiwa kwa kumnyany’anya mfanyabiashara huyo.

Kutoka kushoto: Michael Mbanya Wathigo, Ronald Onyango Otieno na Dishon Peter Mulinge wakiwa kortini Milimani Mei 16, 2018 kwa kumshambulia mfanyabiashara Timothy Muriuki. Picha/ Richard Munguti

Wote walioshtakiwa ni Mabw Mbugua, Mulinge, Otieno, Wathigo, Owino, Antony Otieno Ombok  almaarufu Jamal na Benjamim Odiambo Onyango almaarufu Odhis.

Mshukiwa mwingine wa nane Bw Sangira Stephen Ochola anaendelea kuchunguzwa na polisi ibainike ikiwa alihusika na kisa hicho.

Kiongozi wa mashtaka Bw Solomon Naulikha alimweleza hakimu kuwa “ hapingi Mabw Mulinge,Otieno na Wathigo wakiachiliwa kwa dhamana.”

Alimsihi hakimu awaachilie washukiwa hao kwa masharti ya dhamana kama ya washukiwa walioshtakiwa awali.

“Washukiwa waliofikishwa kortini awali waliachiliwa kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh200,000. Naomba korti iwaachilie washukiwa hawa kwa masharti sawa na hayo,” Bw Naulikha alisema.

Wakili Danstan Omari anayewakilisha washtakiwa hao watatu aliomba korti aamuru akabidhiwe nakala za mashahidi.

Bw Andayi aliwaachilia kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu kila mmoja na kuamuru kesi zote zitajwe Mei 23 ndipo ziunganishwe ziwe kesi moja,

Katika kesi dhidi ya Bw Ochola hakimu alimtaka mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP Noordin Haji awasilishe ushahidi kuhusu madai yanayotolewa kortini badala ya kuacha korti “ itegemee uvumi.”

Korti iliorodhesha kesi kusikizwa Julai 17.

Video Gallery