Makala

WASIA: Dini, kuwapa wanafunzi fursa kujieleza kwaweza kutatua utumiaji vileo

June 26th, 2019 2 min read

Na HENRY MOKUA

KILA mtoto afanyapo mtihani, nia ya mzazi huwa kuona kwamba mwanawe amefanya vema.

Kufanya vema hapa kuna maana kwamba, mwanawe huyo awe amezoa alama nzuri kuliko ya mtihani uliotangulia au mambo yakiwa mabaya zaidi, adumishe alama yake ya awali.

Wapo wanafunzi ambao hujitahidi na kuzidi kuimarika ingawa nao hudumisha matokeo yao wakati mwingine.

Wengine hudumisha matokeo yao daima huku wakiteleza mara mojamoja na kuzoa alama za chini.

Wapo wanaodidimia hatua kwa hatua hadi wakawakatiza tamaa wazazi au waangalizi wao; baadhi ya wanafunzi hawa hawajali kwa hivyo hapana haja ya kusema kwamba nao hukata tamaa ijapo wapo miongoni mwao wanaokata tamaa kweli baada ya kufeli au kufeli kama tokeo la kukata tamaa.

Mwanafunzi anapodidimia masomoni, jambo moja hudumu akilini mwa mzazi, mwangalizi; je, ni kipi kiini cha mwanangu kufeli au kuzidi kufeli? Ikiwezekana kiini cha hali hii kikabainika, mzazi hupata nafuu kidogo.

Ripoti ya uchunguzi wa Nacada iliyotolewa wiki jana kuhusu utumiaji wa vileo miongoni mwa wanafunzi nchini ni tukio muhimu kwa washika dau wa elimu nchini.

Kwa mzazi ambaye hudumu kukisia chanzo cha mwanawe kufeli asikibaini, ripoti hii yaweza kuwa ya msaada kwake kwa kiasi fulani.

Kwa mwalimu ambaye hushuku kwamba pana la mno linalomfanya mwanafunzi wake fulani kutodumisha makini darasani, ripoti hii yaweza kumwangazia na kumwelekeza panapofaa.

Mwanafunzi aliyesikia matokeo ya ripoti hii sasa anajua hatari inayomzunguka iwapo yeye si mtumiaji wa vileo vilivyotajwa.

Mbona niseme hivi lakini? Ni heri unapojua kiini cha tatizo lako kwani waweza kukikabili.

Isitoshe, ripoti ile imeangazia masuala fulani ya kimsingi na yenye mafao makubwa kwa jamii nzima.

Huoni kwamba inashangaza, inashtusha hasa asilimia 72 ya wanafunzi wanapodai kwamba pana uwezekano kwao kutumia vileo walimu wao wasijue?

Ikiwa watavitumia nyumbani au shuleni bila ufahamu wa mwalimu, nani atawanasihi dhidi ya ukiukaji huu wa maadili na kuwaelekeza kuukomesha iwapo tayari wamejiingiza kwao? Je, taarifa kwamba asilimia 32 wanapata dawa hizi kutoka kwa marafiki wao ambao tunatarajia kwamba ni marika yao? Isitoshe, asilimia 29 hubeba vileo hivi kutoka nyumbani, asilimia 22 wakavinunua kutoka baa zilizo karibu na shule zao, na asilimia 16 nyingine kuvinunua kutoka maduka au vioski vilivyo karibu na shule zao.

Jambo jingine la kusikitisha ni kwamba asilimia 48 ya wanafunzi hupata dawa hizi wanapokuwa likizoni, asilimia 35 wanapokuwa njiani kutoka shuleni, asilimia 27 wanapokongamana wakati wa michezo au tamasha, asilimia 24 wakati wa burudani shuleni na asilimia 21 wanapozuru shule nyingine; almuradi hapana mahali panapo salama kwa kizazi hiki kichanga.

Je, masurufu tunayoyahangaikia ili yawafae wanetu wanapokuwa shuleni? Nayo yamedhihirika kuchangia upotovu huu yanapozidi; yaani, tunapowapa hela za matumizi shuleni zaidi ya kiwango kinachostahiki.

Ewe mwalimu, mzazi, usije ukashika tama, ikibidi ufanye vile, na iwe unawazia suluhu. Naam, wahenga walituwekea bayana busara yao kwamba ushikwapo shikamana.

Angalau sasa tumejua uzito wa tatizo letu; kwa msingi huu tuna kila sababu ya kushikamana kulitatua.

Kuithamini dini

Kwanza, mhimize mwanao kuithamini dini, la, ucha Mungu kwa sababu sijaona katika ripoti hii wanafunzi wakitaja kwamba hushiriki vileo katika maeneo ya ibada.

Usidhani kwamba waweza kumhimiza kuenda ibadani ukasalia nyumbani, la, kumhimiza ni kuongoza njia na kumshawishi akufuate.

Jambo moja ambalo nimelibaini katika harakati zangu za kuwanasihi wanafunzi kibinafsi na kuwashauri katika makundi ni kwamba hamna mwanafunzi aliyenasika katika upotovu asiyetaka kujinasua. Hili tulijue kwa hakika.

Kila mwanafunzi ambaye ametekwa na utumiaji vileo akawa mraibu atamani sana kujiokoa, kinachohitajika ni mwongozo.

Hebu katoe mwongozo huo mwenzangu kwa stahamala uone kama hatakushukuru hatimaye.

Nawe mwalimu mkuu na walimu wako wazia masuala ya dini shuleni mwako kama fursa muhimu ya wanafunzi kujieleza na kuweka matatizo yao bayana.

Nakuhimiza ualike mgeni baada ya vipindi mahsusi ili aseme nao uone kama hawatakiri wamenaswa na hapo utapata njia ya kuwasaidia kwani watashauriwa kuhusu namna ya kujinasua.