Makala

WASIA: Kusikiliza kwa makini ni njia hakika ya kuchota maarifa ya kukufaa

March 13th, 2019 2 min read

Na HENRY MOKUA

JE, ni mara ngapi wewe husikiliza unapofahamishwa kuhusu jambo usilolijua?

Je, unapofahamishwa kuhusu ulijualo? Ni mazoea ya wengi wetu kusikiliza kwa nia ya kujibu.

Kusikiliza huku hutufanya kulenga upungufu wa maelezo yanayotolewa ili tuyapinge au kuwa na msingi wa kuyatilia shaka kwa urahisi.

Ni wachache miongoni mwetu waliojifunza kufuatilia maelezo kwa stahamala hadi tamati ndipo tujue iwapo maana inayokusudiwa ni ya moja kwa moja au msemaji katumia mbinu kama kinaya kujieleza ili kukoleza ujumbe wake zaidi.

Hivi, ni kwa nini mtu, hata anayehitaji sana msaada akose kusikiliza kwa makini ili afafanukiwe kuhusu atakalo kulijua?

Bila shaka zipo sababu au tuseme misingi ambayo kwayo mtu aweza kukosa kusikiliza kwa makini.

Mojawapo ni hasira.

Ninapoandika makala haya namkumbuka mzazi mmoja ambaye alikataa kata kata kunisikiliza juzi baada ya kukasirishwa na matokeo duni ya mwanawe pamoja na mwanawe huyo kukosa baadhi ya mitihani.

Baada ya mwanawe kujieleza, kwamba alikosa kufanya mitihani hiyo kwa sababu ya kushiriki mashindano ya michezo, mzazi wake alielekea kupata kibali cha kuwalaumu walimu kwa kutomakinikia matakwa ya wazazi pamoja na wana wao.

Maelezo kwamba wapo wanafunzi wengine walioshiriki mashindano hayo lakini wakafanya mitihani yote hayakumbadili nia – alikwisha kuzomewa na mumewe, akakasirishwa na mwanawe – ilimbidi pia amkasirishe au hata kumbughudhi mtu.

La kusikitisha ni kwamba alitoa mkataa mwanawe asiwahi kushiriki michezo tena wala mashindano ya michezo yenyewe.

Isitoshe, aliwahi kukiri kwamba yeye alicheza vizuri enzi zake lakini hatimaye akawa mtu wa maana.

Ikiwa hujaipata vilivyo maana aliyoikusudia hapa, u sawa na mimi ila naomba tujaribu kuielewa.

Mzazi ninayesimulia kumhusu ni mfano bora wa watu wanaokosa kusikiliza kwa sababu ya hasira.

Hasira zake hazikumruhusu kufafanukiwa kwamba huenda maisha yake yakawa tofauti sana na ya mwanawe. Haihalisi hata kidogo kulalamikia dalili na kuanza kuzitibu.

Ninasema hivi kwa sababu kuna uwezekano mwanafunzi tunayemzungumzia akakoma kushiriki michezo na mashindano ya michezo yenyewe lakini bado akakosa kufanya mitihani.

Kwa hivyo, dalili hapa ni nini na maradhi hasa ni yapi? Madai kwamba kutofanya mitihani kwa mwanafunzi wa kisa na mkasa ni dalili tu ya maradhi yake ya kutomakinika – kisa na maana, wenziwe walioshiriki michezo naye na waliomakinika walihudhuria mitihani ile ile aliyopaswa kuifanya.

Kudhibiti mihemko

Napenda kukuasa ewe mzazi, mwanafunzi, mwalimu na mwanajamii kwa jumla kwamba ni muhimu kudhibiti mihemko yako kila usikivu unapohitajika.

Mihemko ya dakika kadhaa isije ikawa sababu yako ya kutoifikilia ndoto uliyo nayo na hivyo kukuvurugia mustakabali.

Je, ikiwa maisha ya halafu ya mwanafunzi anayekatazwa asishiriki michezo yamening’inizwa kwenye michezo yenyewe, itakuwaje?

Ni kwa kusikiliza walimu ambapo tunaweza kufaana kwa kuelezana kuhusu mbinu zilizothibitika kuleta mafanikio kwa mwanafunzi – kujiona wajua kila lote ni kujitia katika tundu la ukiwa na ulegevu wa kitaaluma. Namna vyuma vinavyonoana ndivyo watu wanavyopanua maarifa na kuibuka kuwa bora zaidi.

Ewe mzazi, waweza kujifunza kutoka kwa mzazi mwenzio iwapo utakuwa radhi kusikiliza nasaha yake. Huenda ikawa suluhisho kwa msongo wako wa miezi kadha au hata miaka.

Nawe mwanafunzi kumbuka ndiwe kiini cha nasaha hizi – msikilize mwalimu wako kwa makini na stahamala, wanafunzi wenzio vilevile; sina shaka utakuja kutusimulia kisa cha ufanisi wako. Kila la heri.