Makala

WASIA: Patiliza changamoto inayokukabili iwe ngazi katika juhudi zako

November 13th, 2019 3 min read

Na HENRY MOKUA

MWANADAMU alipoumbwa hakudekezwa.

Badala yake, alipewa kazi ya kumshughulisha – kumpa changamoto – kazi kabla ya pumziko.

Nakisia haukua mzaha kwake Adamu kuvipa viumbe vyote majina; kuanzia mkewe hadi siafu na viumbe vingine vidogo mno ambavyo kwako na kwangu, ni rahisi kuvisahau. Tukio la kustarehe lilijiri baada ya kazi nyingi tu ambayo ingemlazimu kuhitajia pumziko. Hebu linganisha enzi hizo za uumbaji na sasa… Leo, wengi wetu, hasa vijana – wakiwemo wanafunzi, hutamani kustarehe mfululizo bila kujishughulisha.

Wapo wengine ambao huona kwamba wazazi wana mali ya kutosha kuwarithisha hivyo wakaamua kujidekeza tu wakijua wakijitahidi wasijitahidi, maisha yatawanyookea tu kwani hawatakosa tonge la kutia kinywani. Hata hivyo kuna wachache ambao ni vielelezo kwa namna wanavyojituma, si tu katika mazingira ya kawaida bali pia dhidi ya changamoto kubwa – wakavumbika ndoto zao mpaka zikaiva.

Mmoja wa vijana na wanafunzi wa humu nchini aliye na kila sababu ya kuigwa ni Maryan Noor Yussuf. Binti huyu ambaye alizaliwa jijini alikuwa na ndoto sawa na za mtoto mwengine yeyote; kwamba angeishi na wazazi wake hadi utu uzimani. Mambo yalibadilika ghafla lakini siku moja baba yake alipoondoka nyumbani kikawaida tu asiwahi kurejea. Baba mtu ambaye alikuwa wa kutegemewa kukidhi mahitaji ya familia alipokosa kurejea kwa miezi kadhaa, ilimbidi mtu, ndugu zake na mamaye wahame jijini kwani hata kodi ya nyumba ilikuwa balaa kulipa. Naona unaelekea kuamua kwamba walihamia kwa babu, bibi, amu au shangazi hivi…lakini umekosea. Subiri kidogo nikutaarifu – walielekea katika kambi ya wakimbizi…ah! Wasema kweli msimulizi? Hebu taja jina la kambi yenyewe iwapo si ya kubuni… Je umesikia kuhusu kambi ya wakimbizi ya Kakuma? Enhe! Ile ambayo ipo katika mojawapo ya maeneo maskini zaidi nchini? Naam, hiyo ndiyo naizungumzia.

Kutoweka kwa baba yake asijue endapo yu hai au kafa ulikuwa msingi wa kuandaa mswaada wake wa kitabu kiitwacho: I Will Be Back, yaani, Nitarudi – mswada alioukamilisha akiwa katika darasa la saba! Mswaada huu uliokawia kugeuzwa kitabu kutokana na Maryan kuwaziwa kuwa mtoto pamoja na unyanyapaa, ulipochapishwa hatimaye, Maryan aligeuka kivutio, akawa mhamasishaji mara moja hiyo. Shule jirani na yake zilimtafuta awahimize wanafunzi wazo. Alipougua maradhi ya hiatal hernia ambayo hulifanya tumbo kufura na ambayo nusra yampokonye uhai mwaka jana, yalimchochea kuandika kitabu kingine alichokiita: Nobody Knows My Pain, anwani ninayoweza kutafsiri kama ‘Hamna Ajuaye Uchungu Wangu.’ Hakukomea hapo lakini; tajriba, ujuzi alioupata kutokana na kibarua alichokifanya baada tu ya kuhitimu kidato cha nne ilikuwa msingi tosha wa kuanzisha kampuni yake ya kutalii na kusafiri ambayo ndiye Afisa Mkuu Mtendaji (CEO) wayo katika umri wa miaka 19 tu!

Mbona wewe hujilaza mafua tu yanapokukabili? Mbona unadumu kumlalamikia na hata kumlaani mzazi au mwangalizi wako unapokosa chajio mara mbili tatu? Mbona unamwombea hila mwalimu wako anapokupa mazoezi ya kutosha kuuvumbua uwezo wako uliofichika? Je, mpaka lini utazidi kukitanua kifua kwamba nyinyi – sijui wewe na nani – ni wenye nacho na ukifanya bidii usifanye mustakabali wako ni hakika utang’aa?

Lau kama ungegutuka leo na kujikung’uta – vumbi ikuondoke, utandu na tongo zilizo machoni mwako hali kadhalika…kisha uianze safari yako upya! Katika safari yako mpya, iifanye bidii kuwa desturi yako kwani kwa kuikosa waweza kuchezea kamari mali unayotegemea kurithishwa na katikati ya mwaka mmoja miwili utakuwa ombaomba wa kupigiwa mfano. Jisake kwa makini na kuanza kuziona changamoto kama vidato vya kupandia hadi kuzifikilia ndoto zako.

Ukigundua umeteleza, na naona upo katika harakati hiyo…sema na mtu unayeweza kumwamini ili awe shahidi wa maamuzi yako mapya – akutathmini na kukupa mjibizo baada ya vipindi mahususi hadi yawe mazoea yako kuzigeuza changamoto kuwa msingi wa kubuni mbinu mpya za kuzikabili. Jifunze kuwa na kiasi katika kila jambo; kula, kwa kiasi, kutazama runinga, kwa kiasi, kucheza, kwa kiasi, kupumzika, kwa kiasi, kulala, kwa kiasi.

Baada ya kipindi kifupi kisa chako kitakuwa na mashiko kiasi kwamba kitaangaziwa katika safu hii bila wewe kujua. Hata kisipoangaziwa, utakuwa umewachochea wengi kuyabadili maisha yao kwa njia chanya. Kila la heri!