Makala

WASIA: Udanganyifu ni mkakati hakika wa kujichimbia kaburi kiakademia

July 24th, 2019 2 min read

Na HENRY MOKUA

WAKATI mwingine mimi huketi nikajiuliza kinachomfanya mwanafunzi kufanya udanganyifu katika mtihani, mujarabu au hata zoezi.

Yaani mwanafunzi yule yule anayehangaikiwa na mwalimu na mzazi wake huamua tu kwamba ataingia katika chumba cha mtihani na maandishi anayokisia yana majibu kwa maswali atakayoulizwa.

Mwingine huamua kunakili majibu ya mwenziwe kwa vyovyote vile licha ya hatari inayohusiana na hatua hiyo.

Azma yake huwa kuzoa alama nzuri japo ghushi ili ambabaishe mwalimu na mzazi wake kwamba amemakinika masomoni.

Sijui iwapo mwanafunzi mwenye tabia hii hujaribu kuwazia athari za hulka yake hii!

Kwa kuwa sina hakika wewe unayeshiriki tabia hii wajua madhara yake au labda kuna mwingine anawazia kujaribu kutumia mbinu hii, naomba nikutajie hatari mbili tatu za hali hii.

Pengine umemwona mwanao, mwenzio amenaswa katika hali hii, maelezo haya yatakufaa pia kumnasihi.

Mosi, udanganyifu katika mitihani ni miongoni mwa mambo yanayomkatiza mwalimu tamaa ajabu! Inakuwaje utumie mbinu ghushi wakati mwalimu amejinyima starehe zinazofungamana na umri wake; mustakabali aliokuwa anaungoja siku zote za ujana wake kisha umsaliti kwa kuonesha hakukuandaa vilivyo? Ah! Inakera si haba!

Hivi, mbona uhudhurie vipindi darasani kwanza iwapo umenuia kufanya udanganyifu?

Mbona usijishughulishe na mengine mwalimu anapokuwa darasani badala ya kumsikiliza kwa makini kisha ukamsaliti? Iwapo hukuwahi kujua, ghadhabu anayokuwa nayo mwalimu unapofanya hivi ni kubwa mno!

Je, tokeo la kukasirishwa nawe? Uhusiano wenu wa kikazi huvurugika bila shaka; yaani, mwalimu hukoma kushawishika tena kwa urahisi kukupa msaada wowote uwao ili ufuzu. Nalo hili likifanyika, uwezekano wako wa kufeli huwa mkubwa zaidi.

Pili, wajidanganya mwenyewe. Ukifanikiwa kutekeleza udanganyifu ulioupangia bila mwalimu kujua usifikiri umefika! Hii ni hatua ya wazi ya kujidanganya kwamba unajua kumbe hujui.

Matokeo utakayoyapata mtihani hadi mtihani, mujarabu hadi mwingine hayatakuwa ya manufaa kwako kwa vyovyote vile. Kumbuka, mtihani huwa kigezo cha kupimia uwezo na uelewa wako wa uliyofunzwa kufikia hapo ulipo.

Kwa hivyo, ukipata alama 50 wakati unastahiki 20, hutajua kiasi cha jitihada unazohitaji kutia au juhudi za kuongeza ili ufuzu.

Tatu, wamdanganya mwalimu na mzazi wako. Kwa kawaida, mwalimu anapogundua una udhaifu fulani – na hufanya hivi kupitia mitihani – huweka mikakati, na mapema kuhakikisha anakukwamua. Inakuwaje ukimdanganya umeiva kumbe hujui ta wala be!

Atajiambia umemakinika, umejiandaa vilivyo na hivyo hana sababu ya kukutengea muda wa ziada wa mashauriano.

Mzazi naye hujenga tumaini lisilo na mashiko akilini mwake akijua atapata kivuno kizuri tu kutokana na jasho lake. Hatimaye huwaje? Unafeli na kushindwa hata na masuala mengine ya maisha kwani huwa umezoea njia za mkato.

Mwalimu hushtuka, mzazi vilevile na haiwi vigumu kuwasababishia msongo au hata shinikizo la damu mambo yanapofikia hapa!

Sasa nifanyeje? Swali zuri! Kwanza, kuwa huru kumweleza mwalimu wako hali halisi ya mambo.

Ualimu

Ikiwa hukujua, ualimu ni taaluma inayoambatana na nasaha; mwalimu atakupongeza kwa kukiri kosa na kuamua kubadili mbinu. Atakuelekeza vilivyo kuhusiana na hali yako mahsusi.

Zaidi ya hivyo, jipe kuamini kwamba kila mmoja wetu ameumbiwa uwezo tofauti.

Kwa hivyo, usije ukatishwa na matokeo ya fulani; fanya bidii kwa kiwango chako, kubali matokeo ya bidii yako.

Huenda hili lisiwe rahisi kama kunena lakini jifunze hivyo.

Wengi walioubadilisha ulimwengu ni waliojiamini na kuridhishwa na waliyowezeshwa na Mwenyezi Mungu kuyafanya, hawakuwa bora zaidi ukiwalinganisha na wenzio.

Tambua vipengele, masomo unayoyamudu na kuyadhibiti vizuri kwa msaada wa mwalimu yasije yakakuponyoka.

Hatimaye, tambua udhaifu wako na kutafuta msaada miongoni mwa wanafunzi wenzio, walimu ili kuutatua.

Utaipenda hali yako mpya, utajiwekea msingi wa ushindi wa halali ambao hutawahi kuujutia. Jaribu ujionee!