Makala

WASIA: Ukiitumia vyema likizo unaweza kubadili kabisa mustakabali wako

August 7th, 2019 2 min read

Na HENRY MOKUA

BARAKA alikuwa mwana wa kutegemewa sana na baba yake aliyekuwa amekonga kwani walimzaa katika uzee wao.

Baada ya kifo cha mamaye, baba mtu alisalia naye kama tegemeo la pekee katika siku zake za uzeeni.

Zaidi ya kujiambia mara kwa mara kwamba Baraka ndiye wa kumfaa kwa lolote lile, angemtajia Baraka hili pia asije akamtelekeza.

Mara nyingi, mwana huyu ambaye alikuwa baraka hasa sawa na jina lake, alimtii na kumsaidia baba yake kadri ya uwezo wake.

Kumtuma Baraka karibu au mbali kulikuwa kawaida tu, na siku moja, kwisha kuvamiwa na njaa, baba mtu alimtuma sokoni akanunue vyakula na aandae chamcha.

Baraka alishika njia na kulenga alipotumwa. Kama kawaida, hakujiruhusu kushiriki michezo waliyokuwa wakijishughulisha nayo wenziwe.

Alifika sokoni na kununua kila alichotumwa na kuanza kurejea nyumbani.

Wakati huu ndio kwanza alilimbuka kuona mchezo waliokuwa wakiucheza wenziwe umeshika kasi.

Alikumbuka mara moja alivyokuwa mchezaji bora na wenziwe hawakusita kumwingiza mchezoni.

Aliwaachia mashabiki wa timu aliyonuia kuichezea vyakula alivyokuwa amevinunua na kuingia uwanjani.

Aligeuka nyota kwa kipindi kifupi, akawa tegemeo la timu aliyojiunga nayo.

Walicheza, wakacheza na kucheza hadi saa ya kurejea nyumbani ikawadia. Hapo ndipo alikumbuka kutwaa vyakula alivyokuwa amenunua ili akimbie navyo nyumbani.

Ajabu ni kwamba mchezo ulipokamilika tu watu walifumkana wakaelekea kila upande asiweze kupata bidhaa zake; chakula hana! Hela za kununua kingine hana! Baba yake yu taabani nyumbani…

Hii ikiwa likizo ya mwisho kwa watahiniwa wa Cheti cha Kuhitimu Masomo ya Msingi na kile cha Sekondari, maswali ni mengi wanayouliza watahiniwa hawa.

Muhimu zaidi lakini, sawa na Baraka, wengi wanajiuliza: mchezo ukamilikapo, sharti kurejea nyumbani; nitarejea na nini?

Hatua

Kwako mtahiniwa unayejiuliza utarejea nyumbani na nini? Una nafasi ya pekee katika siku kadhaa hizi za likizo yako kubadilisha mambo.

Kwanza, hakikisha umejiandaa vilivyo kwa angalau masomo mawili hivi uyapendayo ili ujizidishie nafasi ya kufuzu vyema, kurejea nyumbani na kitu cha haja.

Yaweza kuwa Hisabati na Kiswahili, Dini na Sayansi, Kemia na Jiografia (kwa wanafunzi wa shule za upili); yazamie masomo haya kuhakikisha unazoa alama za juu zaidi mtihani wa kitaifa uwadiapo.

Ikiwa wewe ni mtahiniwa wa shule ya msingi, ukipata asilimia 80 katika masomo mawili, utakuwa na alama 160 tayari.

Kupata asilimia 60 tu katika kila mojawapo ya masomo matatu yaliyosalia, utaibuka na 180 nyingine.

Hii ni sawa na alama 340/500 jumla – alama ya kukuwezesha kujiunga na shule ya upili ya ndoto zako. Ikiwa wewe ni mtahiniwa wa sekondari, A mbili ni sawa na alama 24.

Ukizipata, utakuwa umesaza 22 tu kujiunga na chuo kikuu; ina maana kwamba ukiongeza C- mbili na D+ tatu, utakuwa umetimiza matakwa ya kimsingi ya kujiunga na chuo kikuu. Mbona urejee nyumbani mikono mitupu mchezo ufikiapo tamati? Hili liwazie tena na tena.

Jinyime na kupitia yote yanayokujuzu katika somo unaloliona jepesi. Fanya mashauriano ya kina na walimu, wajuzi wa somo, masomo hayo.

Yaangazie hali kadhalika yale unayoyaona mazito katika kipindi hiki – usiyapuuze. Yapo pia ya lazima na ya kimsingi; usisite kuyatia maanani. Kuimarisha matokeo yako katika Kiswahili na Kiingereza, soma vitabu viteule kwa mara nyingine katika likizo hii ewe mtahiniwa wa sekondari.

Kwa hivi, utakumbuka msuko au mtiririko wa mawazo kwa urahisi na hivyo kujibu swali lolote lihusulo vitabu viteule vilivyo katika Fasihi ya Kiingereza na ile ya Kiswahili. Matokeo haya yatakuwa muhimu katika masomo haya mawili kwa jumla.