Habari Mseto

Wasia wa mfu utakuwa ukizingatiwa utata ukiibuka – Mahakama

August 6th, 2019 2 min read

NA MAUREEN KAKAH

MAHAKAMA Kuu juzi ilitoa uamuzi ambao unaheshimu wasia wa marehemu kuhusu anakofaa kuzikwa iwapo utata utaibuka na kusema tamaduni haifai kuzingatiwa kamwe.

Jaji Jesse Njagi alisema uamuzi wa marehemu kuhusu namna na anakofaa kuzikwa unafaa kuheshimiwa licha ya uwepo wa tamaduni za jamii mbalimbali zinazotoa mwelekeo kuhusu suala hilo.

“Ni jukumu la mahakama kutumia sheria za kitamaduni panapo haja na isipowezekana inafaa kuzingatia masuala yote yanayozingira utata wa mazishi kabla ya kutoa uamuzi,” akasema Jaji Njagi.

Aidha alidai kwamba hakuna sheria kwenye katiba inayotoa mwongozo kuhusu namna ya kutatua mizozo ya mahala pa kuzika marehemu nchini.

Kesi iliyochochea uamuzi wa Bi Njagi ilihusisha mzozo wa watoto wa mwanamke aliyeaga dunia mwaka jana waliokuwa wakipigania mahala pa kumzika mzazi wao.

Kwenye kesi hiyo, wanawe marehemu Stella Auma Odawa walitofautiana kuhusu mahali pa kumzika ikizingatiwa kwamba aliolewa kwa mumewe Dixon Odawa katika Kaunti ya Vihiga na wakajaaliwa watoto saba kabla ya ndoa yao kutibuka miaka ya 60.

Bi Odawa baadaye alihamia kwa mwanawe moja Samuel Ochieng’ eneo la Kibos Kaunti ya Kisumu hadi alipofariki Julai mwaka jana. Kufuatia kifo chake, kifungua mimba wake, Morris Odawa alielekea kortini kumzima Bw Ochieng’ dhidi ya kumzika mama yao, akitaka marehemu asafirishwe na kuzikwa kwa mumewe.

Ingawa hakimu alitupilia mbali kesi yake, Bw Morris alielekea katika mahakama kuu na kukata rufaa akisema sheria kuhusu utata wa mazishi ilifasiriwa vibaya.

Kulingana na Bw Morris, hakimu huyo alitoa uamuzi usiofaa wa kuzuia mwendazake kuzikwa kwenye boma la mumewe, mahali ambapo wanawe wengine wamekuwa wakiishi.

Bw Morris alifafanulia korti kwamba kulingana na tamaduni za jamii ya Waluo, mwanamke ambaye hujaliwa watoto na mumewe kisha kuachana kutokana na mafarakano kwenye ndoa huzikwa kwa mume huyo anapofariki.

Vile vile, Bw Morris alidai kwamba wazee walijadili suala hilo na kuafikiana kwamba mamake alifaa kupumzishwa kwa mumewe kwa sababu tamaduni ya Waluo haitambui talaka. Aliomba mahakama ibatilishe uamuzi wa awali wa hakimu.

Hata hivyo, Bw Ochieng’ alieleza korti kuwa mamake alimweleza akiwa hai kwamba akifariki, azikwe kwenye makazi yake mapya alikoishi baada ya kuachana na mumewe.

Bw Ochieng’ alidai kwamba itakuwa fedheha na ukiukaji wa haki kwa korti kulazimisha mazishi ya mamake yaandaliwe mahali ambapo aliondoka zaidi ya miaka 50 iliyopita. Pia alidai tamaduni ya Waluo hailingani na katiba na mapenzi ya marehemu mamake.

Japo hakimu alimruhusu Bw Odawa kushiriki kwenye mipango ya mazishi ya mkewe, alikataa kutoa idhini mwili wake uzikwe kwa mumewe.

“Korti lazima izingatie hoja zote na itoe uamuzi wa haki. Haitakuwa vyema kuzika mwili wa mwendazake katika boma lake la zamani alikotoka na hata hakurejea akiwa hai,” uamuzi wa hakimu ulieleza.