WASIA WA NDOA: Utafanyaje ndoa ikikosa kuridhisha?

WASIA WA NDOA: Utafanyaje ndoa ikikosa kuridhisha?

NA BENSON MATHEKA

UMEINGIA katika ndoa ukiwa na matarajio makubwa ya kutimiziwa ahadi ulizopatiwa.

Mke anasubiri mumewe amweke maisha ya malkia na watoto wake kuishi kama wana wa mfalme katika mazingira mazuri.

Mume anatarajia kuwa na mke anayemheshimu, kumhudumia, kumzalia watoto wanaokubaliana kabla ya harusi na kumchukulia kama kichwa cha familia.

Lakini punde au baada ya muda katika ndoa, hali inabadilika na matarajio yote yanatoweka. Maisha yanakuwa kinyume kabisa na ulivyotarajia au kwa ufupi, yanabadilika kuwa jehanamu.

Hii ni hali ya kawaida japo haifai kuwa ya kawaida.

Kawaida kwa sababu hali ya maisha hubadilika na kwenda kinyume na mipango au matarajio ya mtu kutokana na mabadiliko yasiyoweza kuepukika. Hivyo basi, kabla ya kuhukumu mumeo au mkeo kwa kukosa kukutimizia matarajio yako, changanua hali mliyopitia au iliyomkumba.

Inawezekana ukawa umechangia katika hali unayojipata ya kukosa kutimiziwa uliyonuia kupata katika ndoa. Hapa, inanikumbusha kitu kingine muhimu; lengo la mtu kuingia katika ndoa. Ikiwa lengo lako ni kuwa na mtu wa kukutimizia, basi kaka na dada utapata mshtuko. Kutimiziana ndilo neno linalopaswa kuwa katika akili na mioyo ya kila mtu anayeingia katika ndoa. Hebu nifafanue hili; ndoa ni ya wenzi, washirika wawili walio na hisa sawa, hivyo basi wanapaswa kufahamiana, kutegemeana, kusaidiana, kufurahishana, kufaana, kutunzana, kuburudishana, kuheshimiana, kushauriana, kuwasiliana na kudekezana.

Haya yote yakikumbatiwa na mume na mke, yanazaa kuridhishana katika hali zozote na hivyo basi suala la kukosa kutimiziwa matarajio linayeyuka.

Mushikili huzuka pale mtu anapotumia vitisho, ugomvi na hulka zingine kulalamikia kutotimiziwa ahadi. Kufanya hivi ni kuharibu mazingira yanayowezesha ahadi unazodai kutimizwa. Ugomvi, vitisho na kuteta ni sumu kwa ndoa na huondoa mazingira ambayo yangetumiwa kukabili hali na kuirekebisha.

Ndoa ikiwa kandarasi inayokusudiwa kudumu maisha yote ya wanaokubaliana kuwa mume na mke, ni wazi kuwa hakuna muda uliowekwa wa kutimiziwa matarajio au ahadi.

Hivyo, ulichoahidiwa kinaweza kutimizwa wakati wowote katika maisha ya ndoa yenu.

Kuna watu wanaooana na kisha mambo yanawaendea kombo na baada ya kuvumiliana hali inarejea ya kawaida na hata kuwa bora zaidi.

Hivyo basi, usihukumu mumeo au mkeo kwa kukosa kukutimizia matarajio yako badala yake, msaidie kupata uwezo wa kutekeleza jukumu lake.

Ikibidi umkumbushe, hakikisha kuna mazingira bora ya kufanya hivyo na usiwahi kumsukuma kufanya linalozidi uwezo wake ukitaka akutimizie matarajio ya ndoa.

  • Tags

You can share this post!

FATAKI: Ajabu kuu ‘wife material’ kuwa mwanamke...

KCSE: Wakuu wa shule Kisii, Nyamira watetea matokeo yao bora

T L