Makala

WASIA: Yadumishe macho na akili yako kwenye mustakabali wako

March 11th, 2020 2 min read

Na HENRY MOKUA

MWANAFUNZI kwa kawaida huwa na maswali kadha, baadhi ambayo huyabana yasijulikane mpaka anapokuwa na uhusiano wa karibu na mwangalizi wake.

Si kwamba ni maswali ya kibinafsi au yanayosheheni siri zisizopaswa kujulukana bali maswali anayoona ni mepesi kiasi kwamba hayafai kuulizwa. Yoshua hajasazwa.

Baada ya kusema naye mara kadhaa, amethubutu kuniuliza: ‘Hivi nawezaje kuudumisha mshawasha nilio nao wa kufanikiwa katika mtihani wangu wa kitaifa na maishani kwa jumla?’

Si swali nililolitarajia, lakini nilifurahishwa nalo kwa sababu lilinihakikishia kwamba Yoshua ni mwanafunzi mwenye hisia na mihemko ya kiuanafunzi; yaani, anaweza kukiri kwamba wakati huwadia mwanafunzi anaona hapana haja ya kukazania ufanisi masomoni kwani hata baadhi ya waliokosa ufanisi huo wamefanikiwa maishani.

Unachosahau ewe mwanafunzi ni kwamba unapopoteza nafasi wazi kabisa kama uliyo nayo uwezekano mkubwa ni wa kujiunga na waliofeli maishani. Kisa na sababu, fursa ya wazi unayojua hakika kwamba ni fursa umeipoteza, itakuwaje utambue fursa za halafu zitakazokujia?

Jambo la kwanza nililofanya ni kumpongeza Yoshua. Yalivyo maumivu kwa mtu anayeugua ukoma ndivyo zilivyo changamoto kwa mwanafunzi. Mgonjwa wa ukoma huyathamini maumivu kwa sababu ndiyo humkumbusha au kumhakikishia kwamba bado yu hai…

Mwanafunzi anapopitia changamoto za kihalisia kama hizi unajua ni mwanafunzi makinifu na yupo radhi kupata nasaha za kihalisia za kumsaidia kuzipiku changamoto zake. Ni kwa msingi huu nilimpongeza Yoshua.

Nawe ikiwa umefikia mahali fulani katika safari yako ya ufanisi ukahisi kwamba umechoka kukazania ufanisi ulio mbali kule…pongezi kwako!

Baada ya kumpongeza, nilimnasihi ayadumishe macho yake na akili yake kwenye maisha anayonuia kuishi katika mustakabali wake miaka michache ijayo. Picha ya nyumba atakayo kuishi kwayo, ofisi anayonuia kufanya kazi kwayo, huduma anazonuia kutoa kwa wateja wake na yote mazuri anayoyatazamia baada ya kupata alama anayoiwania na kusomea taaluma ya ndoto zake.

Msingi wa nasaha hii ni kwamba kwa kawaida tunaiona mistakabali yetu kupitia kwa picha za akilini. Uwezekano mkubwa ni kwamba ndoto zetu za miaka michache iliyopita ndizo zimetufikisha hapa; na ndoto zetu za leo zitatufikisha tutakapo kwenda.

Hii ina maana kwamba unaweza kuishi katika mustakabali wako tangu sasa kwa imani. Ukiiambatanisha imani hiyo na mikakati mwafaka, mambo hutengenea nawe ukawa katika nafasi nzuri ya kuzifikilia ndoto zako hatua kwa hatua. Isitoshe, unakuwa na nguvu mpya kila uchao kwa kutumainia mustakabali wenye kukuridhisha zaidi.

Jambo jingine linalokupasa kufanya ewe mwanafunzi sawa na Yoshua, ni kuungana na mwanafunzi mwenye maono sawa na yako, mwenzi ambaye anaweza kukubebea mzigo, kukuwajibisha – nawe ukafanya vilevile. Huu ni mkakati hakika wa kupiga hatua mbele kwani binadamu ana mazoea ya kuwa mvivu.

Ukimpata mwanafunzi mwenza anayekukumbusha mikakati yako, akakukumbusha shabaha na malengo yako mkasaidiana hapa na pale kupata matokeo mnayostahiki, kufuzu katika mitihani kunakuwa sehemu ya maisha yenu. Kwa hivyo mtafute mwanafunzi wa namna hii mkasaidiane kujiwekea shabaha, kuibuka na mikakati mwafaka ya kuzifikilia shabaha zenyewe na kuzitekeleza shabaha hizo vilivyo!

Mwisho na muhimu zaidi, mtafute mtu atakayekuwa kielelezo kwako. Huyu ni mtu ambaye unaona amefanikiwa katika yale unayoyawania na labda ni mtaalamu katika taaluma unayotazamia kuisomea. Mwombe akushike mkono. Tembea naye. Mweleze changamoto unazozipitia mara kwa mara. Safiri naye. Dumu naye kadri inavyowezekana.

Aghalabu tunakata tamaa tunapokumbana na changamoto hii na ile kwa sababu tunafikiri ndisi wa kwanza kuipitia. Ninavyoshuhudia mara kwa mara ninaposema na baba yangu mzazi, nyingi za changamoto zangu ni marudio ya changamoto alizozipitia alipokuwa katika umri wangu wa sasa. Ninapokuwa nimemweleza jambo ninaloliona zito ajabu, husafisha koo kisha akaanza: ‘Heri wewe…hali yangu ilikuwa mbaya zaidi!’

Baada ya maelezo yake ya kushadidia changamoto yake ilivyokuwa kubwa, hubaki nimeachama tu. Huwa ninapata nguvu mpya haswa. Nawe sema na mtu unayeweza kumwaminia mustakabali wako. Utashangaa changamoto zako zitakavyokuwa nyepesi!