Habari MsetoSiasa

Wanasiasa 34 wandani wa Ruto watisha kugura chama cha Jubilee

March 10th, 2019 1 min read

DENNIS Lubanga na TITUS OMINDE

WABUNGE wanne wa bunge la kitaifa na wakilishi wadi 30 kutoka Kaunti ya Elgeyo/Marakwet wametishia kukihama chama cha Jubilee iwapo rais Uhuru Kenyatta hataondoa siasa katika vita dhidi ya ufisadi hasa katika mabwawa ya Kimwarer na Arror.

Wabunge Bowen Kangogo, (Marakwet Mashariki), William Kisang (Marakwet Magharibi), Daniel Rono (Keiyo South), Jane Chebaibai (Mwakilishi wa Wanawake) na Spika wa bunge la kaunti Bw Philemon Sabulei ambaye aliwakilisha wabunge 30 kutoka katika bunge la kaunti hiyo walisema vita hivyo vinatumiwa kisiasa kwa lengo la kumdunisha naibu rais Dkt William Ruto.

Kwa pamoja, walimtaka rais Uhuru Kenyatta kuamrisha uchunguzi sawa na huo kufanyiwa mabwawa mengine kote nchini ambayo yanafadhiliwa na serikali.

Miongoni mwa mabwawa hayo ni Thwake, Mukuyuni miongoni mwa mengine.

Spika wa bunge la Elgeyo Marakwet Bw Philemon Sabulei alisema madai ya ufisadi yanayoelekezwa mabwawa ya Kimwerer na Arror, yanaongozwa na siasa za ubinafsi wala si vita dhidi ya ufisadi.

“Kuna mabwawa mengi nchini ambayo yanafadhiliwa na serikali mbona ni mabwawa yetu tu ndio yanalengwa, hivi ni vita vya kisiasa ambavyo vinalenga naibu rais Dkt William Ruto,” alisema Bw Sabulei

Bw Sabulei alidai kuwa vita hivyo vinalenga kuzima azma ya naibu kuelekea Ikulu 2022. Wakihtubia wana habari katika hoteli ya Boma Inn mjini Eldoret walitaka rais Uhuru Kenyatta kuelekeza vita sawa katika mabwawa mengine iwapo anapigana na ufisadi.

“Kuna mabwawa mengine katika ngome ya rais Kenyatta ambayo yana matatizo sawa na mabwawa yetu kwa nini tusione vita kama hivyo katika mabwawa hayo, mbona ni mabwawa ya ngome na naibu rais tu ndiyo yanavamiwa,” alisema Bw Kangogo Bowen mbunge Keiyo Mashariki.

Kwa pamoja walitaharadhirisha rais Kenyatta dhidi ya kutomfuta kazi waziri Henry Rotich.

Bw Bowen alisema Bw Rotich ambaye amekuwa akihojiwa na idara ya upelelezi kuhusiana na ufisadi akitaka mabwawa hayo ambayo anatumika kama njia ya kudunisha naibu rais.