Habari za Kaunti

Wasichana 10 wakesha seli baada ya kukeketwa, saba wakiokolewa


WASICHANA 10 katika lokesheni ya Giika, eneo la Igembe Kusini Kaunti ya Meru, Jumatatu, Agosti 12, 2024, walikesha seli baada ya polisi kuendesha msako dhidi ya ukeketaji.

Polisi pia walimkamata ngariba ambaye inadaiwa alipatikana akiwapasha tohara wasichana hao pamoja na wazazi wao.

Miongoni mwa waliokamatwa ni chifu msaidizi aliyejaribu kuficha kisa hicho kwa kuwaficha wasichana wawili waliokeketwa na kuzuia kukamatwa kwa washukiwa hao.

Chifu wa Lokesheni ya Giika, Bw Gervase Mucheke,  ambaye aliongoza oparesheni ya  kuzima sherehe hiyo haramu ya ukeketaji Jumapili usiku, alisema wakeketaji wengine wawili  walitoroka.

Bw Mucheke,  alisema wasichana 17 walikamatwa katika msako huo lakini saba hawakuwa wamepashwa tohara.

“Tulipata habari kutoka kwa umma Jumapili na tulifanya uvamizi usiku. Tathmini ya kimatibabu imethibitisha kuwa wasichana 10 walikeketwa. Inaonekana wengine saba walikuwa wakingoja kukeketwa,” Bw Mucheke alisema.

Alisema mmoja wa wapashaji tohara waliotoroka, amekuwa akiendesha kituo cha afya katika eneo hilo ambaye anaaminika kuwa daktari feki.

“Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yamefanya kampeni dhidi ya ukeketaji katika eneo hili. Uovu huu ulikuwa umeisha kwa miaka mingi hadi likizo hii. Bado hatujabaini ni nini kimeanzisha wimbi hili jipya la ukeketaji,” chifu huyo alisema.

Bw Mucheke alisema polisi walikuwa wakimtafuta tabibu huyo ambaye anaaminika kuwatahiri wasichana katika kliniki yake.

Alisema washukiwa hao kwa sasa wanatoza ada ya hadi Sh2,500 kwa  kila msichana wanayepasha tohara.

Mwanaharakati anayepinga ukeketaji Meru, Bi Catherine Thiakunu, alikashifu kisa hicho na kutaka visa hivyo vifuatiliwe hasa wakati  huu wa likizo ya Agosti.

“Inasikitisha kwamba wahusika wa ukeketaji kwa mara nyingine tena wanatumia wakati wa likizo ya shule kuwapasha tohara wasichana wetu. Inasikitisha pia kwamba hata maafisa wa utawala wanaunga mkono uovu huu kwa kuwaficha waathiriwa. Kuna haja ya kuongeza uhamasishaji wa jamii ili kukomesha uovu huo,” alisema.